Mgodi wa dhahabu waporomoka Sudan na kuwaua watu 6
6 Septemba 2025Mkurugenzi wa eneo la Berber Hassan Ibrahim Karar, amesema juhudi zinaendelea za kuwaokoa watu walionasa kwenye vifusi lakini hakutaja sababu ya kuporomoka kwa mgodi huo.
Tangu mapigano yalipozuka nchini Sudan mnamo mwezi April mwaka 2023 kati ya jeshi na vikosi vya RSF, pande zote mbili zimekuwa zinafadhili vita hivyo kupitia uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Vyanzo rasmi na mashirika yasiyo ya kiserikali yamesema karibu biashara yote ya dhahabu ya nchini Sudan inaendeshwa kupitia Umoja wa Falme za Kiarabu, nchi ambayo imekuwa inalaumiwa kwa kuwapa silaha wapiganaji wa vikosi vya RSF. Hata hivyo Umoja wa Falme za Kiarabu unakanusha vikali tuhuma hizo.
Kwa upande wao wataalam wa madini wameeleza kuwa sehemu kubwa ya dhahabu inayozalishwa na pande zote mbili zinazopigana inasafirishwa kwa njia ya magendo kupitia Chad, Sudan Kusini na Misri kabla ya kuingia Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo kwa sasa ni nchi ya pili duniani kwa usafirishaji dhahabu nje.