MEXICO CITY : Israel yataka kushinikizwa kwa Iran
12 Machi 2005Israel imesema hapo Ijumaa kwamba Iran inakaribia kuwa na uwezo wa kutengeneza bomu la nuklia na kuitaka Marekani na Ulaya kuishinikiza serikali ya Tehran kutelekeza mpango wake unaoshukiwa kutengeneza silaha za nuklea.
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Silvam Shalom ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba bomu la nuklea la Iran litakuwa jinamizi kwa Israel na kwa nchi nyengine duniani.
Shalom amekaririwa katika mahojiano wakati wa ziara yake nchini Mexico akisema kwamba kwa maoni yao wako karibu sana, karibu mno kuwa na maarifa ya kutengeneza bomu la aina hiyo na ndio sababu inabidi kuchukuliwe hatua ya haraka.
Pakistan ilikiri wiki hii kwa mara ya kwanza kwamba mwanasayansi alieingia fedhehani kwa kuhusika na biasahara ya magendo ya nuklia aliipa Iran mashinepewa ambazo zinaweza kutumika kutengenezea silaha za nuklea.
Hapo jana Iran imesema bado kuna utata juu ya masuala kadhaa muhimu baada ya mazungumzo ya siku nne na mataifa ya Umoja wa Ulaya kuhusu shughuli za nuklea za Iran.
Kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo yaliomalizika Ijumaa huko Geneva Sirus Nasseri amesema licha ya jitihada zao zote hawakuweza kufikia muafaka kwa vile utata bado ungalipo katika masuala kadhaa muhimu.
Nasseri amesema wataendelea kuzalisha nishati yao ya nuklea kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa taratibu za kimataifa na kwamba kitu pekee wanachoweza kuwapatia wajumbe hao wa Ulaya ni hakikisho kwamba shughuli zao hizo hazitokuwa kwa ajili ya kijeshi.
Wakati huo huo Marekani imekubali kuipatia Iran vifuta jasho vya kiuchumi ili nchi hiyo iachane na mpango wake huo wa nuklea. Uingereza,Ufaransa na Ujerumani zimesema zitaifikisha Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iwapo itaanza tena kurutubisha uranium na shughuli za nishati ya nuklea ambapo vinaweza kutumika kutengenezea silaha za nuklea.