Merz: Urusi itawekewa vikwazo ikipuuza mchakato wa amani
9 Mei 2025Merz ameyasema hayo Ijumaa akiwa ziarani mjini Brussels, Ubelgiji atakapokutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO Mark Rutte na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya.
Kando ya kitisho cha vikwazo kwa Urusi, Merz amesisitiza kuwa Ulaya inaunga mkono mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha vita kwa siku 30 kati ya Urusi na Ukraine.
Akizungumza katika ziara yake ya kwanza mjini Brussels tangu alipoapishwa kuwa kansela mpya wa Ujerumani, Merz amesema Umoja wa Ulaya na Marekani zitaendelea kuiunga mkono Ukraine na kuiongezea misaada kama itahitajika japokuwa Ujerumani inaendelea kuupinga mpango wa deni la pamoja la Umoja wa Ulaya ili kufadhili bajeti ya ulinzi.
Merz amesema mataifa kadhaa ya Ulaya ikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Poland na Uingereza, yako tayari kuunga mkono mpango huo wa Trump kwa tamko la pamoja.
Kansela Merz, ambaye ameingia madarakani wiki hii ameahidi kuifanya Ujerumani isikike tena barani Ulaya na duniani kote. Alipokuwa kiongozi wa upinzani, Merz aliahidi kuumaliza ukimya wa Ujerumani kwa sera ya Ulaya na kumlaumu Kansela aliyepita Olaf Scholz kwa kutumia njia hiyo wakati wa uongozi wake.
Merz akanusha tangazo la hali ya dharura kuhusu uhamiaji
Merz yuko ziarani mjini Brussels ambako tayari ameshakutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Antonio Costa. Akizungumza pamoja na Costa, Merz amewahakikishia washirika wake kwa kuapa kuwa ataendelea kufanya kazi ''kulingana na sheria za Ulaya''.
Amepanga pia kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, na Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola.
Kabla ya kukutana na viongozi hao Kansela Merz amezungumza na waandishi habari na kuweka wazi kuwa hakuna mtu yeyote katika serikali ya Ujerumani aliyeitangaza hali ya dharura kuhusiana na suala la uhamiaji. Ametoa kauli hiyo kukanusha ripoti iliyoandikwa na gazeti la Ujerumani la Welt.
Hata hivyo, amesema kwa sasa serikali yake inafanya ukaguzi wa kina mipakani kwa kuzingatia sheria kama ilivyokuwa wakati wa mashindano ya kuwania ubingwa wa Ulaya yaliyofanyika mwaka uliopita.
(AFP, DPA, Reuters)