Merz: Putin anaona mazungumzo ya amani 'dhaifu'
26 Mei 2025Merz ameliambia shirika la utangazaji la umma WDR, ni wazi kuwa Putin anaona mapendekezo ya mazungumzo hayo kama dhaifu, na kwamba juhudi za kidiplomasia za kuumaliza mzozo wa Ukraine zimekumbana na hatua kali za kijeshi kutoka Moscow. Kulingana na Merz, washirika wa Ukraine kutoka nchi za Magharibi, wametumia kila njia za kidiplomasia zilizopo.
Amebainisha kuwa watu wanaoiunga mkono Ukraine wamefanya kila kitu walichoweza. Merz ameonya ikiwa hata pendekezo la pande hizo mbili kukutana Vatican halijapata idhini ya Putin, basi wanatakiwa wajitayarishe kuona vita hivyo vikidumu kwa muda mrefu, kuliko wanavyotamani kuviona vinamalizika.
Ukraine saa ina makombora ya masafa marefu
Aidha, kansela huyo wa Ujerumani amesema washirika wa Magharibi hawaweki tena marufuku na mipaka ya aina mbalimbali za silaha kwa Ukraine, na kwamba nchi hiyo sasa ina makombora ya masafa marefu kuweza kuilenga miundombinu ya kijeshi nchini Urusi.
''Hakuna tena vikwazo vya silaha zinazotolewa kwa Ukraine, sio kutoka kwa Uingereza, wala Ufaransa, wala sisi, na wala Marekani. Hii inamaanisha kuwa Ukraine sasa inaweza pia kujilinda yenyewe, kwa mfano kwa kushambulia maeneo nchini Urusi. Haikuweza kufanya hivyo, hadi hivi karibuni. Sasa inaweza,'' alifafanua Merz.
Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema anadhani Rais wa Marekani Donald Trump sasa anatambua uongo wa Putin kuhusu Ukraine. Macron ameitoa kauli hiyo baada ya Trump kusema kuwa Putin amekuwa 'mwendawazimu' kutokana na kuendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine, na hivyo alikuwa anafikiria kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi.
Macron amesema ana matumaini kuwa hasira ya Trump dhidi ya Urusi itabadilika na kuwa vitendo. Akizungumza Jumatatu akiwa ziarani Vietnam, Macron amesema sasa Trump amegundua kuwa Putin alimdanganya.
Zelensky kuzuru Ujerumani
Wakati huo huo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky anatarajiwa kuizuru Berlin siku ya Jumatano, kukutana na Merz. Gazeti la Ujerumani, Der Spiegel, limeripoti Jumatatu kuwa Merz anataka kujadiliana hatua zinazoweza kuchukuliwa kuelekea katika mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi. Merz anatarajiwa kumuarifu Zelensky kuhusu mipango ya vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, vinavyonuwia kuongeza shinikizo kwa Moscow kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Huku hayo yakijiri, Mkuu wa ujasusi wa kigeni wa Ukraine, Oleh Ivashchenko amethibitisha taarifa kwamba China inaipatia bidhaa muhimu Urusi katika viwanda vyake vya kijeshi. Ivashchenko amesema Jumatatu kuna taarifa kwamba China inaipatia Urusi bidhaa maalum za kemikali, baruti, unga wa risasi na vifaa vingine vinavyoiwezesha kutengeneza risasi. China imekanusha madai hayo, ikisema hayana msingi.
(AFP, DPA, AP, Reuters)