Merz azidisha shinikizo kwa EU kuhusu magari ya umeme
9 Septemba 2025Merz alitoa wito huo Jumanne wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya magari ya IAA mjini Munich, ambapo wazalishaji wakubwa wa Ulaya wamesisitiza umuhimu wa EU kutathmini upya mpango huo unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makampuni makuu ya Ujerumani kama VW, BMW na Mercedes-Benz pamoja na muungano wa Marekani-Ulaya, Stellantis yameeleza hofu kuhusu kasi ya mabadiliko, wakikabiliana na ushindani mkali kutoka kwa watengenezaji wa China kama BYD.
Merz, ambaye alichukua madaraka mwezi Mei, hakupinga moja kwa moja marufuku ya 2035, lakini alisema anataka kanuni za Ulaya ziwe "smart, thabiti na rahisi zaidi.” Aliongeza kuwa kulazimisha teknolojia moja ni sera mbovu kiuchumi: "Tunataka kulinda mazingira kwa njia yenye gharama nafuu kupitia uwazi wa kiteknolojia.”
Kiongozi wa jimbo la Bavaria, Markus Söder – mshirika wa kisiasa wa Merz – alizungumza kwa ukali zaidi: "Marufuku ya injini za mwako ni kosa. Tunahitaji chaguo mbadala kwa sababu injini bado zina nafasi. Umeme utashinda muda mrefu lakini tunahitaji muda zaidi kuandaa Ulaya.”
Wasiwasi wa viwanda na ajira
Hotuba hizo zimepokelewa kwa faraja na baadhi ya wafanyakazi wa sekta ya magari. Jan Vlasak, mhandisi wa programu katika kiwanda cha Ujerumani, alisema amefurahi kuona wanasiasa wakiegemea sekta hiyo. Alipendekeza marufuku ya 2035 isogezwe mbele kwa angalau miaka mitano au kumi.
Hata hivyo, sekta ya magari barani Ulaya inakabiliwa na changamoto kubwa. Pamoja na uwekezaji mkubwa katika magari ya umeme, mauzo yamekuwa madogo kuliko ilivyotarajiwa. Aidha, gharama za uzalishaji nyumbani zimepanda huku ushindani kutoka China ukizidi kuongezeka.
Kulingana na ripoti ya EY, sekta ya magari ya Ujerumani tayari imepoteza zaidi ya ajira 50,000 mwaka uliopita. Volkswagen inapanga kufuta nafasi 35,000 kufikia 2030 na kusitisha uzalishaji katika viwanda viwili. Porsche, Audi na mamia ya wasambazaji wa vipuri nao wameshaweka mipango ya kupunguza wafanyakazi.
Merz amesema atakutana na viongozi wa sekta hiyo hivi karibuni ili kutafuta njia ya kulinda nafasi ya Ujerumani kama kiongozi wa uzalishaji duniani.
Shinikizo kutoka China
Wakati huo huo, zaidi ya kampuni 150 za magari ya umeme zimeandika barua ya wazi kwa Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen zikimtaka "kutolegeza” lengo la 2035. Wakati maonyesho ya IAA yakihitimishwa Ijumaa, makampuni ya magari yanatarajiwa kukutana naye mjini Brussels kujadili mustakabali wa sekta hiyo.
Kwa mwaka huu makampuni ya magari ya China yamekuja kwa wingi kuliko ya Ulaya. Kati ya kampuni 700 zinazoshiriki IAA, 100 zinatoka China – ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na maonyesho ya 2023. BYD, ambayo imeongeza mauzo yake barani Ulaya kwa kasi, imewasilisha gari lake jipya Dolphin Surf kwa bei ya euro 20,000, na kuanza uzalishaji katika kiwanda kipya nchini Hungary ili kuepuka ushuru wa EU.
Volkswagen nayo imejibu kwa kutangaza modeli mpya za bei nafuu ili kushindana na wimbi la magari kutoka Mashariki.
Chanzo: AFPE