Merz atilia shaka marufuku ya vyama vya siasa kama AfD
15 Mei 2025Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, ameonyesha mashaka kuhusu pendekezo la kukipiga marufuku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland (AfD), ambacho hivi karibuni kiliorodheshwa kama "chama cha siasa kali za mrengo wa kulia" na idara ya ujasusi ya ndani ya nchi hiyo, ingawa hatua hiyo inasubiri uamuzi wa rufaa ya kisheria.
"Nina mashaka kila mara na mchakato wa kupiga marufuku vyama vya siasa," Merz aliambia gazeti la Die Zeit siku ya Alhamisi.
"Na kila mara nimeepuka kuanzisha mchakato wa aina hiyo kutoka nafasi ya wastani bungeni. Huo ni mfano unaoashiria nia ya kuwaondoa wapinzani wa kisiasa," aliongeza Merz.
Soma zaidi:Maandamano dhidi ya itikadi kali za mrengo wa kulia yaenea vijijini
Mwisho wa Aprili, Idara ya Ujasusi wa Ndani ya Ujerumani (BfV) iliitangaza AfD kuwa "kundi la siasa kali za mrengo wa kulia lililothibitishwa," ingawa haitatumia rasmi jina hilo hadi rufaa ya chama hicho itakaposikilizwa mahakamani.
Uthibitisho usiyo na mashaka ni muhimu
Merz alisisitiza kwamba ni lazima kuthibitishwa kuwaAfD inafanya kazi kwa njia "ya uchokozi na ya kupambana dhidi ya mfumo wa demokrasia huria na wa kikatiba wa Ujerumani." Alisema mzigo wa uthibitisho huo uko mikononi mwa serikali kuu, na si bunge.
Katika uamuzi wake, BfV ilisema kuwa sera za AfD zinaeleweka kwa misingi ya "ukabila na asili ya kizazi" na zinadhalilisha makundi fulani ya watu nchini Ujerumani na kukiuka heshima ya utu wao.
Soma pia: Ujerumani yasitisha lebo ya itikadi kali dhidi ya AfD
Ingawa AfD hupata takriban asilimia 20 ya kura kwenye tafiti za maoni, vyama vikuu vya siasa vya Ujerumani kama CDU cha Merz na chama cha Social Democrats (SPD) cha mrengo wa kati-kushoto vimekataa kushirikiana nacho kwa njia ya mkataba wa kisiasa au muungano wa serikali.
Wengi wa Wajerumani wanaamini kuwa ajenda ya AfD inapingana na demokrasia, utawala wa sheria na utu wa binadamu. Hata hivyo, suala la namna bora ya kukabiliana na chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia linaibuka kama hoja inayoweza kuligawanya zaidi taifa hilo.