Merz anataka ushuru wote kati ya Marekani na Ulaya uondolewe
9 Mei 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ametaka ushuru wote kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya uondolewe. Ni wakati wa mazungumzo yake kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump.
Akizungumza Ijumaa mjini Brussels akiwa pamoja na rais wa baraza la Ulaya Antonio Costa, kansela Merz amesema amemwambia Trump hafikirii ni wazo zuri kuuchochea mgogoro huo kuhusu forodha.
Akiwa ziarani mjini Brussels, Merz ameliunga mkono wazo la Trump la kipindi cha siku 30 cha usitishaji mapigano nchini Ukraine bila masharti na ametahadharisha kuhusu kuiwekea vikwazo zaidi Urusi kama haitatoa ushirikiano.
Merz anatarajiwa kukutana na katibu mkuu wa NATO Mark Rute, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa bunge la Ulaya Roberta Metsola.
Mazungumzo ya NATO yanatarajiwa kutuwama kuhusu vita vya Ukraine na utayari wa muungano huo wa kijeshi kuvikabili vitisho vya Urusi.
Ziara ya Merz inafanyika kabla mkutano wa kilele wa NATO mwezi ujao mjini The Hague, utakaokuwa wa kwanza kumjumuisha rais Donald Trump wa Marekani tangu aliporejea madarakani Januari mwaka huu.