Merz aapa kujenga jeshi imara zaidi barani Ulaya
14 Mei 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema serikali mpya inayovijumuisha vyama vya Christian Democratic Union CDU, Christian Social Union, CSU, na chama cha Social Democratic, SPD, inafahamu fika kuhusu changamoto kubwa za ndani ya nchi na kimataifa, hasa kuhusiana na fedha za umma.
Merz amesema watafanya kila wawezalo kuurudisha uchumi wa Ujerumani kwenye njia ya kukua, huku akikabiliana na mlolongo wa mipango kabambe kuanzia kuifanyia matengenezo miundombinu ya nchi hadi kupunguza viwango vya kodi vya mashirika.
Hata hivyo Merz amesisitiza kwamba Ujerumani ina nguvu na inaweza kutegemea kazi kwa bidii, ubunifu na kujitolea kwa dhati kwa watu wake, akiongeza kuwa serikali mpya imeshawishika kwamba Ujerumani inaweza kuzishinda changamoto inazozipitia wakati huu yenyewe na kuzigeuza kuwa kitu kizuri.
Ahadi yake ya ufunguzi kuhusu mafanikio kwa wote ilikuwa ni ishara ya kukubaliana na sera za waziri wa zamani wa uchumi na kansela wa Ujerumani Ludwig Erhard aliyemwagiwa sifa kwa kuuchochea uchumi wa Ujerumani na kuinasua nchi kutokana na mdororo wa kiuchumi baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, na ambaye aliandika kitabu kwa jina "Prosperity for All" - "Mafanikio kwa Wote."
Kansela wa Ujerumani aapa kuuimarisha tena uchumi
Kansela Merz amesema serikali yake italenga kulifanya jeshi la Ujerumani liwe na nguvu kubwa kabisa barani Ulaya katika wakati ambapo kuna hali ya sintofahamu na kukosekana uhakika katika siasa za dunia. Amesema serikali yake itatenga fedha za kutosha zinazohitajika kwa ajili ya majeshi yake.
Kansela Merz auzungumzia mzozo wa Ukraine
Merz amesema atafanya kila jitihada kuendelea kuimarisha umoja kadri inavyowezekana kati ya washirika wa Ulaya na Marekani kuhusiana na vita vya Ukraine na jinsi ya kuvifikisha mwisho. Amesema ni muhimu kwamba nchi za Magharibi zisiruhusu kugawanywa, huku viongozi wa Ulaya wakiahidi vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi.
Merz amesema nchi za Magharibi hazitakubali amani ya kulazimishwa kwa Ukraine wala kukubali hali iliyosababishwa na vikosi vya Urusi.
Alikuwa akizungumza siku moja kabla wajumbe wa Ukraine na Urusi kukutana kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta amani mjini Istanbul nchini Uturuki hapo kesho Alhamisi, ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu tangu kuanza kwa mgogoro mbaya kabisa wa umwagaji damu barani Ulaya tangu kufika mwisho kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Baada ya kushinda uchaguzi Februari, kansela Merz aliahidi kuipa Ujerumani jukumu kubwa zaidi katika rubaa ya kimataifa na kuliimarisha jeshi lake kwa kutenga fedha zaidi za matumizi ya kijeshi.
Ingawa ameukosoa wazi utawala wa rais wa Marekani Donald Trump kama mshirika asiyeweza kutegemewa, Merz amemshukuru Trump kwa msaada wake katika kushinikiza usitishaji mapigano nchini Ukraine. Amesema usitishaji mapigano unaweza kufungua mwanya ambapo mazungumzo ya kutafuta amani yanaweza kufanyika.
Merz amesema vita vibaya vya Ukraine na matokeo yake havitaamua tu ikiwa sheria na utangamano vitaendelea kuwepo barani Ulaya na ulimwenguni kote, ama ikiwa dhuluma, nguvu za kijeshi, na haki kamili ya walio na nguvu zaidi itashinda.