Juhudi za kutafuta washirika wa serikali mpya zaanza Berlin
25 Februari 2025Friedrich Merz aliwasili katika ofisi ya kansela mjini Berlin kwa majadiliano hayo ambayo yanatarajiwa kujadili kipindi cha mpito kabla ya kuundwa kwa serikali ijayo. Merz, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Scholz kama kansela mpya wa Ujerumani, baada ya chama chake cha CDU na chama ndugu cha Bavaria CSU, kupata ushindi wa asilimia 28.5 ya kura, katika uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumapili (23.02.2025). Chama cha Scholz cha Social Democrats (SPD) kilichopata matokeo mabaya kwa kuibuka cha tatu kwa asilimia 16.4 ya kura, kinatarajiwa kuwa mshirika mdogo katika serikali ya Merz.
Katika harakati za kuipanga serikali yake tayari kansela huyo mtarajiwa ameshaweka wazi kwamba serikali yake, haitofanya mageuzi yoyote katika sheria iliyojumuishwa kwenye katiba ya nchi, inayoweka ukomo kwa serikali kuchukua mkopo zaidi ya kiwango kilichokubalika. Merz amesema suala hilo ni pana linalohitaji bunge jipya kulijadili na kufikia uamuzi.
Viongozi duniani wampongeza Merz kwa ushindi
Tukirejea katika harakati za kuunda serikali mpya, awali Scholz alisema hatokuwa na jukumu lolote katika mchakato au mazungumzo ya kuunda serikali, ila atabakia tu kuwa kiongozi wa mpito hadi serikali mpya itakapochaguliwa. Anapanga pia kujiondoa katika nafasi zote za uongozi na kubakia tu kama mwanachama katika bunge la Ujerumani Bundestag.
Hata hivyo mwenyekiti mwenza wa SPD Lars Klingbeil amechukua usukani katika mazungumzo ya kuunda serikali ambako inaarifiwa amekwishakutana na Merz jana Jumatatu. Kabla ya kansela huyo ajae wa ujerumani Friedrich Merz, kukutana na Scholz, kwanza alikutana na viongozi wakuu katika muungano wa vyama ndugu CDU/CSU akiwemo Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Söder, katibu Mkuu wa CDU Carsten Linnemann na Kiongozi wa wabunge wa CDU/CSU Thorsten Frei.
SPD: CDU itupe hakikisho la kutoshirikiana na AFD kabla ya kuwa mshirika katika serikali mpya
Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani la ZDF, Lars Klingbeil alisema SPD hakitositisha jukumu lake kitakapoitwa kuungana na vyama vingine kuunda serikali, lakini pia akatahadharisha kuwa chama hicho kisilaumiwe patakapotokea mvutano katika mazungumzo hayo huku akisema ni jukumu la chama kilichopata ushindi kuhakikisha mazungumzo hayaendi mrama.
Ikumbukwe kwamba wakati wa mdahalo wa wagombea wa ukansela kabla ya uchaguzi wa bunge kufanyika, Friedrich Merz alitupiana maneno na mwenzake Olaf Scholz baada ya CDU kupendekeza uwepo wa sheria kali za uhamiaji na SPD nayo ikionya kuwa sheria hizo sio halali chini sheria ya Ujerumani.
Matokeo ya Uchaguzi wa Ujerumani katika michoro
Chama cha SPD chake Kansela Scholz kitataka kwanza hakikisho kutoka kwa CDU chake Merz, kwamba kinajitenga kwa uwazi kabisa na chama cha siasa kali cha AFD, kabla ya kutia saini makubaliano ya aina yoyoteya kuwa mshirika katika serikali mpya ya muungano nchini Ujerumani.
Chama hicho cha AFD kilipata asilimia 20.8 ya kura katika uchaguzi wa bunge, matokeo yaliyokiingiza kwa mara ya kwanza bungeni. Kulingana na makubaliano katika siasa za Ujerumani ni marufuku kwa chama chochote kushirikiana na AFD kuunda serikali.
dpa