Mazungumzo ya kitaifa DRC bado ni kitendawili
26 Agosti 2025Mpango huo wa amani shirikishi nchini Kongo ambao ni matokeo ya mikutano kadhaa ya kiufundi, unalenga kumaliza mzunguko mbaya wa migogoro ya kivita ambayo imeikumba nchi hiyo kwa miongo mitatu.
Tangu ulipopendekezwa miezi saba iliyopita na viongozi wa makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti nchini humo bado kuna kiwingu katika mpango huo.
Katika tamko lao, viongozi wa madhehebu hayo ya kidini wamemtaka rais wa Kongo Felix Tshisekedi kuchukua hatua kwa mujibu wa katiba ili kuzindua rasmi mchakato huo haraka iwezekanavyo.
Lakini hadi sasa mchakato huo umekwama na rais Tshisekedi ambaye mwanzoni alionekana kusita kuuunga mkono, hatimaye ameteua timu ya wataalam ili kutathmini kwa kina maudhui ya mpango huo uliopendekezwa.
Kutoaminiana kwa wadau wa mchakato huo
Lakini changamoto bado ni kubwa kwani kuna hali ya kutoaminiana. Serikali ya Kinshasa haina imani na makanisa ambayo ndio waanzilishi wa mpango huo huku upinzani nao ukiwa hauiamini serikali.
Chama tawala cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kingependa kutumia fursa hiyo kujadili matatizo yanayoikabili DRC , hasa suala la kubadilisha katiba. Lakini chama tawala kinahofia kuwa mazungumzo hayo huenda yakatumiwa vibaya. Adolphe Amisi Makutano wa chama cha UDPS amewataka wadau wote kwanza kuaminiana.
" Kwanza kabisa, watu wanaopendekeza mchakato huu wa mazungumzo ya kitaifa ni lazima kwanza waweze kuaminiana baina yao. Lakini vitendo vinavyoshuhudiwa na waanzilishi wa mchakato huu hasa maaskofu havijengi misingi ya kuaminiana."
Mtazamo wa upinzani wa Kongo
Kwa upande wake, muungano wa Lamuka unaoongozwa na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kongo Martin Fayulu , unasisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo hayo kutokana na migogoro ya kijamii, kisiasa na kiusalama inayoikabili DRC. Hata hivyo Lamuka wanashuku kuwa serikali wana ajenda ya siri kama anavyoeleza Prince Epenge, msemaji wa muungano wa upinzani wa Lamuka.
" Tunapata hisia kuwa utawala wa Tshisekedi unaahirisha mazungumzo haya ili kujipatia muda zaidi. Tunashuku kwamba nia yao ni kuanzisha mazungumzo kwa nia ya kuendeleza muda wa uongozi, ilhali kwetu sisi, tunazingatia zaidi suala la kumaliza haraka vita hivi vinavyogharimu maisha ya watu."
Mpango huo wa kuanzisha mchakato wa mazungumzo ya kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umejikita katika kuanzisha hali ya kuaminiana na kumaliza mifarakano ya kisiasa , kuweka misingi ya kiufundi na kitaalam ili kuwezesha mchakato huo, kuwaleta pamoja wadau wa kitaifa kuhusu masuala ya amani na kukuza suala la kuishi pamoja kwa amani katika eneo la Maziwa Makuu.
// DW Kinshasa