Mazungumzo ya Urusi na Ukraine yafanyika Istanbul
16 Mei 2025Hayo yalikuwa mazungumzo ya mara ya kwanza tangu mashauriano ya mwanzo yalipovunjika mnamo wiki za mapema baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.
Mazungumzo hayo mjini Istanbul, nchini Uturuki yalidumu kwa muda usiozidi saa mbili na kila upande umetoa mtazamo tofauti kuhusu kilichojadiliwa.
Ukraine imeituhumu Urusi kupuuza mwito wake wa kusitisha vita kwa muda mapigano na kudai kwamba Moscow imeleta matwaka mapya mezani ya kuilazimisha Ukraine iondoe vikosi vyake kwenye maeneo makubwa ya ardhi yake.
Hayo yameelezwa na afisa mmoja wa Ukraine ambaye hakutaka jina litajwe.
Urusi yenyewe imesema imeridhishwa na siku ya kwanza ya majadiliano na iko tayari kuendelea na mazungumzo. Inaarifiwa kwenye mazungumzo ya leo pande hizo mbili zimekubaliana kubadilishana wafungwa wapatao 1,000.