Mazungumzo ya Putin na Witkoff yalikuwa "muhimu"
6 Agosti 2025Haya ni kwa mujibu wa msaidizi wa sera za kigeni wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Yuri Ushakov.
Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi imezidisha mashambulizi yake ya angani, droni na hata ardhini dhidi ya Ukraine huku Rais Volodymyr Zelensky akiitaka Marekani kuiwekea shinikizo zaidi Urusi ili ikubali usitishwaji wa mapigano.
Ikulu ya Kremlin ilichapisha ukanda wa video uliomuonyesha Rais Putin akisalimiana kwa mkono na Witkoff wakati wa kuanza kwa mkutano huo.
Mkutano huo umedumu kwa karibu muda wa saa tatu ukiwa na nia ya kupata suluhu kwa mzozo huo uliodumu kwa miaka mitatu na nusu kufuatia Urusi kuivamia Ukraine.
Ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Washington
Msaidizi wa sera za kigeni wa Kremlin, Yuri Ushakov alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo amesema;
"Yalikuwa mazungumzo muhimu na yenye kujenga. Linapokuja suala la mada, kwanza mzozo wa Ukraine umejadiliwa na mada ya pili ilihusu uwezekano wa kuunda ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Washington. Kwa upande wetu, kuna ishara zilizotolewa hasa katika suala la Ukraine. Kulikuwa na ishara pia kutoka kwa Rais Trump kuhusu suala hilo," alisema Ushakov.
Ushakov lakini amekataa kutoa taarifa zaidi hadi pale Witkoff atakaporipoti kwa Trump kuhusiana na jinsi mkutano wake na Putin ulivyokwenda.
Mjumbe wa uwekezaji wa Urusi Kirill Dmitriev ambaye awali alimpokea Witkoff ameandika kwenye mtandao wa kijamii akisema "mazungumzo yatashinda." Hakuna tamko lolote lililotolewa kutoka upande wa Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alijinasibu kuwa atavimaliza vita vya Ukraine ndani ya saa 24 baada ya kuingia ofisini, ameipa Urusi hadi Ijumaa kupiga hatua mpya za kupatikana kwa amani au ikabiliwe na vikwazo vipya.
Awamu tatu za mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul zimeshindwa kupata mwafaka wa usitishwaji wa mapigano huku pande hizo mbili zikitofautiana pakubwa katika masharti yao.
Kwengineko Urusi imeyazidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine ikiilenga miundombinu muhimu na maeneo yanayokaliwa na raia kote kusini mwa nchi hiyo Jumatano.
Majengo ya kibiashara na makaazi kuharibiwa
Mamlaka za Ukraine zimeripoti shambulizi la droni la Urusi katika kiwanda kimoja muhimu cha kusindika gesi katika eneo la Odessa.
Waziri wa Nishati wa Ukraine Svitlana Brynchuk amelaani shambulizi hilo akisema Urusi inatumia namna na uwezo wake wote kuuharibu uwezo wa Ulaya kujitegemea katika masuala ya nishati.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imethibitisha kufanyika kwa mashambulizi katika mfumo wa usafirishaji gesi wa Ukraine ila haikutaja hasa eneo mashambulizi hayo yalikofanyika.
Mashambulizi zaidi ya Urusi yameharibu majengo ya kibiashara na makaazi katika eneo la Dnipropetrovsk na kulingana na maafisa wa Ukraine, mashambulizi ya droni yameyalenga maeneo ya Danube kusini.
Ukraine imekuwa ikijilinda dhidi ya uvamizi kamili wa Urusi uliofanyika Februari mwaka 2022 ambao umelemaza kabisa uzalishaji wa gesi, nchi hiyo sasa ikitegemea ununuaji wa bidhaa hiyo muhimu kutoka mataifa ya kigeni.
Vyanzo: Reuters/AFP/DPA