Mazungumzo ya nyuklia ya Iran yakamilika bila mafanikio
27 Agosti 2025Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghai, ameiambia televisheni ya taifa kuwa pande hizo mbili zilibadilishana maoni wakati wa mkutano wa Geneva. Bila mafanikio, mzozo juu ya mpango tata wa nyuklia wa Iran una hatari ya kuongezeka kisiasa. Mwezi mmoja uliopita, wawakilishi wa serikali kutoka Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, wanaojulikana kwa pamoja kama E3, walikutana na wajumbe wa Iran huko Istanbul. Lengo lilikuwa ni kuongeza shinikizo la kisiasa kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ili kuusukuma uongozi wa Iran kuelekea kwenye makubaliano ya kidiplomasia.
Mataifa ya Ulaya yametishia kurejesha vikwazo vya zamani vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ikiwa suluhisho la mzozo wa nyuklia halitapatikana kufikia mwishoni mwa Agosti. Baghai amesema kuwa kwa mtazamo wa Iran, kurejeshwa tena kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa sio haki.