Mazungumzo ya mkataba wa plastiki yaendelea Geneva
5 Agosti 2025Hii ni mara ya sita kwa wajumbe wa kimataifa kukutana kujadili mkataba huo, na matarajio ni kwamba huu uwe mkutano wa mwisho kabla ya makubaliano rasmi kufikiwa mwishoni mwa mwaka 2024.
Tofauti kubwa katika mazungumzo haya ni iwapo mkataba huo utajumuisha kupunguza uzalishaji wa plastiki, hatua ambayo inapingwa vikali na baadhi ya mataifa yenye uchumi unaotegemea uzalishaji wa mafuta, kama vile Saudi Arabia.
Mataifa haya yanasisitiza kuwa suluhisho linapaswa kulenga kubuni bidhaa zinazoweza kuchakatwa na kutumia tena, badala ya kudhibiti uzalishaji wake moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, zaidi ya nchi 100, baadhi ya mashirika ya mazingira na kampuni kubwa za biashara, wanataka mkataba huo uambatane na hatua thabiti za kupunguza uzalishaji wa plastiki kutoka chanzo, wakisisitiza kuwa kuchakata pekee hakutoshi kuzuia madhara yanayoletwa na plastikikatika mazingira.
Madhara ya moja kwa moja
Angelique Pouponneau, mjumbe kutoka Seychelles na mwakilishi wa mataifa 39 ya visiwa vidogo na maeneo ya pwani yaliyo hatarini, amesema plastiki inaathiri moja kwa moja maisha yao kwa kuharibu samaki, fukwe, na kuua utalii ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wao.
Mjumbe wa wanaharakati wa shirika la mazingira la Greenpeace, Graham Forbes katika mazungumzo hayo ya Geneva amesema:
"Ujumbe wetu kwa viongozi wa dunia ni kusimama imara na kukabiliana na sekta ya mafuta ya kisukuku, wakatae shinikizo kutoka kwa baadhi ya nchi chache zinazojaribu kuzuia maendeleo, na wakubaliane juu ya mkataba madhubuti utakaounda dunia yenye afya na usalama kwa kila mtu.”
Athari za zaidi
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Inger Andersen, alionya kuwa hali ya sasa ya uchafuzi wa plastiki inazidi kuwa mbaya, huku takwimu zikionyesha kuwa kati ya tani milioni 19 na 23 za plastiki huingia baharini kila mwaka. Bila hatua madhubuti, kiwango hiki kinaweza kuongezeka kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2040.
Mnamo Machi 2022, mataifa 175 yaliridhia kutengeneza mkataba wa kwanza wa kisheria kuhusu plastiki, ambao unashughulikia mzunguko mzima wa plastiki — kutoka uzalishaji, matumizi, hadi utupaji. Hata hivyo, mazungumzo ya awali yamekuwa yakikwama kutokana na mgawanyiko kuhusu hatua za kudhibiti uzalishaji.
Mazungumzo mjini Geneva yataendelea kwa siku 10, yakihusisha mawaziri kutoka zaidi ya mataifa 80, mashirika ya mazingira, wanasayansi, makampuni ya biashara, na viongozi wa jamii za asili wanaoathiriwa moja kwa moja na uchimbaji wa mafuta na uzalishaji wa plastiki.