CDU/CSU na SPD zaanza rasmi mazungumzo ya kuunda serikali
13 Machi 2025Hatua hiyo imepigwa baada ya mazungumzo ya awali ya hivi karibuni ambapo kambi ya Christian Democratic Union (CDU, Christian Social Union (CSU) na chama cha Social Democratic (SPD) vilifanikiwa kukubaliana katika masuala muhimu.
Majadiliano ya Alhamisi yanahusisha vikundi 16 ambavyo kila kimoja kina wawakilishi kutoka kwa vyama hivyo vitatu. Wawakilishi wa vikundi hivyo watajadili kwa kina mpango wa kuunda serikali ya pamoja. Wamepangiwa kukutana kwa siku kumi katika majadiliano yatakayoratibiwa na kikosi kazi kmaalumu. Kisha kazi yao itapelekwa kwa kundi kuu katika majadiliano hayo litakalowahusisha viongozi wa kila chama.
Baada ya hapo, rasimu ya makubaliano ya muungano yatapelekwa mbele ya vyama hivyo kwa ajili ya kuidhinishwa. Tayari chama cha SPD kimeshatangaza kuwa kitataka kuwahusisha wanachama wake katika rasimu hiyo. Kiongozi wa CDU Friedrich Merz, anayetazamiwa kuwa Kansela amesema anakusudia kuwa na serikali mpya katikati mwa mwezi Aprili.
Soma zaidi: Merz ataka kuunda serikali haraka
Wakati huohuo, kiongozi huyo wa CDU anautetea mpango wake wa kuongeza matumizi ya ulinzi na miundombinu wakati bunge likianza kujadili mapendekezo yake. Mjadala wa huo wa bunge unaanza leo; na kura ya kuamua kuhusu kuyaunga mkono mapendekezo hayo au kuyakataa itapigwa Jumanne wiki ijayo.
Mipango ya Merz itafanikiwa kupita bungeni?
Licha ya mapendekezo yake kusifiwa na washirika wa Ujerumani nje ya nchi, Merz anakabiliwa na kibarua kigumu kuyapitisha bungeni. Moja ya vizingiti atakavyotakiwa kuvivuka ni kuungwa mkono na Chama cha Kijani. Awali chama hicho kilitishia kuikwamisha mipango hiyo. Ieleweke kuwa, pendekezo la Merz litakihitaji chama hicho katika kulipitisha ili kupata theluthi mbili ya kura.
Wiki iliyopita Merz aliiweka wazi mipango hiyo ya kuongeza bajeti ya ulinzi na miundombinu na kuapa kuwa kambi yake ya CDU na CSU pamoja na washirika wake wanaotarajiwa kuunda serikali ya pampoja wa SPD vitaiharakisha kabla ya bunge la sasa kumaliza muda wake.
Mahusiano dhaifu ya Ulaya na Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump yamechochea miito kwa Ujerumani kuharakisha kuongeza bajeti ya jeshi wakati matumizi ya miundombinu yakionekana kama njia ya kuitoa Ujerumani kwenye mkwamo wa kiuchumi.