Mazungumzo ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza yashika kasi
29 Machi 2025Afisa mmoja mwandamizi wa kundi la wanamgambo la Hamas Bassem Naim, amesema mazungumzo kati ya kundi hilo la Kipalestina na wapatanishi kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano yanashika kasi huku Israel ikiendeleza operesheni kali huko Gaza.
Afisa huyo ambaye ni mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema katika taarifa yake kuwa mazungumzo hayo yanalenga "kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha vita, kufunguliwa kwa vivuko na kuruhusu misaada ya kibinadamu."Mashambulizi ya Israel yauwa watu 70 huko Gaza
Duru za Kipalestina zilizo karibu na Hamas zimelialeza shirika la habari la AFP kwamba mazungumzo hayo yalianza Alhamisi jioni kati ya kundi la wanamgambo na wapatanishi kutoka Misri na Qatar ili kufufua makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachilia mateka Gaza.
Usitishaji wa mapigano dhaifu ambao ulileta utulivu wa wiki kadhaa katika Ukanda wa Gaza ulimalizika mnamo Machi 18 wakati Israeli iliporejelea kampeni yake ya mashambulizi katika ukanda huo.