Marekani yataka kibali cha kuchimba madini ya Ukraine
21 Februari 2025Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Ukraine ambaye anaufahamu wa kinachoendelea kuhusu mazungumzo hayo kati ya Marekani na nchi yake, amesema hivi sasa Kiev inasubiri jibu la Marekani,na kwamba mazungumzo yamekuwa yakiendelea kuhusu, Marekani kupatiwa kibali cha uchimbaji madini nchini Ukraine.
Taarifa hizi zimeibuka katika kipindi ambacho wiki hii rais wa Marekani alimkosoa sana rais Volodymry Zelensky akimuita Dikteta ambaye anaweza kuhatarisha kuipoteza kabisa nchi yake ikiwa hatoitisha uchaguzi na kukubali kuleta amani.
Rubio atetea mazungumzo ya Marekani na Urusi na shutma dhidi ya Zelensky
Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Mike Waltz amesikika akisema kwamba ukosoaji huo wa Trump kwa Zelensky unaakisi kukasirishwa kwa serikali mjini Washington kunakoonekana kama kizingiti kinachosababishwa na Kiev katika kupatikana suluhisho la kuumaliza uvamizi wa Urusi katika taifa hilo la Ukraine.
Lakini pia Marekani imekasirishwa na kukataliwa kwa ombi lake ambalo lingefanikisha kupatiwa mamlaka ya uchimbaji madini Ukraine kwa kubadilishana na hatua ya kuihakikishia ulinzi Ukraine. Na kufuatia hali hii, mvutano kati ya mataifa hayo mawili unaonesha kuongezeka huku washirika wa Ukraine barani Ulaya wakipaza sauti za kuitetea Ukraine.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy amesema Urusi haina haja na amani.
Macron asema Trump hapaswi kuwa dhaifu mbele ya Putin
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye Jumatatu (24.02.2025) anakutana na rais Donald Trump katika ikulu ya White House amesema anapanga kumwambia waziwazi kiongozi huyo kwamba hapaswi kuwa dhaifu mbele ya Vladmir Putin
“Kimsingi hiyo ndiyo sababu kwanini nakwenda Washington kwa siku chache.Kikubwa hapa kinachoonekana ni,kuwepo hali ya mashaka. Trump anatengeneza hali ya mashaka kwa wengine kwasababu anataka kutafuta makubaliano.Kwa hivyo Trump anatengeneza mazingira ya kumfanya Putin kutokuwa na uhakika na hilo kwetu sisi ni jambo zuri. Na kwa kweli hicho ndicho kinachofanyika. Donald Trump ameingia na serikali yake mpya na rais wa Urusi anamtazama na hajui nini atakifanya na anajuwa anaweza kufanya chochote.Hali hiyo inajenga mashaka.Na kwa hakika hii hali ya mashaka ni nzuri kwetu sisi na kwa Ukraine,'' alisema Emmanuel Macron.
Trump amuita Zelensky "Dikteta ambaye hakuchaguliwa"
Kwahivyo rais Macron, akielekea Marekani Jumatatu,siku ambayo kimsingi ni kumbukumbu ya miaka mitatu tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, viongozi wengine wa ngazi za juu katika Umoja wa Ulaya wataelekea Kiev.
Rais wa Halamshauri kuu ya Umoja huo wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa baraza la Ulaya Antonio Costa watakuweko Kiev kwa maadhimisho hayo, pamoja na waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez. Urusi nayo inaendelea kuyateka maeneo zaidi ya Ukraine. Hivi leo imesema imenyakuwa vijivi viwili zaidi mashariki mwa Ukraine katika mkoa wa Donetsk,huku wanajeshi wake wakikaribia kufikia katikati ya mkoa wa Dnipropetrovsk.