Mazungumzo ya amani Gaza yapiga hatua muhimu- Doha
11 Julai 2025Mmoja wa maafisa waandamizi wa Israel amesema kuwa Israel na Hamas wanaendeleza mazungumzo magumu ambayo si ya moja kwa moja huko Doha, akiongeza kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kunaweza kuchukua hadi majuma mawili.
Afisa huyo aliendelea kubainisha kuwa ikiwa pande zote zinazohasimiana zitakubaliana na mpango wa kusitisha vita kwa siku sitini, kunaweza kufungua nafasi ya kuendeleza mazungumzo ya usitishwaji wa kudumu wa mapigano.
Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zilikubaliana Hamas kuwachilia mateka kumi wa Israel inayowashikilia katika awamu mbili na miili ya wengine kumi na nane, kwa sharti kwamba Israel itawaachilia baadhi ya wafungwa wa kipalestina ikiwemo wale waliohukumiwa maisha, huku idadi kamili na majina kuamuliwa katika kikao kijacho.
Suala tete la misaada lilikuwa ni miongoni mwa ajenda ngumu katika mazungumzo hayo, ambapo Hamas ilipinga vikali mfumo unaopigiwa chepuo na Marekani na Israel na badala yake, mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa yameruhusiwa tena kuendeleza usambazaji wa misaada ya kibinadamu Gaza.
Wakati huo huo wapatanishi kama vile Marekani na Qatar wanaendelea kutafuta suluhu juu ya agenda ya uwepo wa kijeshi wa Israel katika njia ya Morag na katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza.
Licha ya maendeleo hayo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel iko tayari kwa makubaliano ya kudumu lakini kwa sharti, Hamas inyang'anywe silaha na ijiondoe kwenye mfumo wa serikali Ukanda wa Gaza.
"Hamas iweke chini silaha zake, vikosi vya kijeshi viondoleze Gaza na Hamas isiwe na mamlaka kijeshi ama kisiasa, haya ndio masharti yetu ya msingi."
Netanyahu aliongeza kuwa "kama tutafanikisha kufikia hayo kwa njia ya mazungumzo, yatakuwa ni mafanikio makubwa. Lakini kama hayo hayatawezekana ndani ya masiku sitini, tutafanikisha kwa njia nyingine-- kwa kutumia nguvu za jeshi letu la kishujaa."
Hamas imelaani matamshi ya Netanyahu na kuituhumu Israel kwa kuyakataa mapendekezo yake.
EU: Tutaweka vikwazo kwa Israel
Umoja wa Ulaya unapanga kampeni ya kuiwekea Israel shinikizo iwapo makubaliano mapya ya misaada kwa Ukanda wa Gaza yatashindikana.
Mkuu wa sera za kigeni Kaja Kallas, amewasilisha kwa nchi wanachama orodha ya hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Israel ikiwa ni pamoja na kusitisha ushirikiano wa kibiashara, na hata vikwazo kwa wanasiasa wa Israel wanaohusishwa na janga la kibinadamu Gaza.
Ndani ya Gaza nako Shirika la Ulinzi wa Raia limesema mashambulizi ya anga ya Israel yamesababisha vifo vya takriban watu sita kaskazini mwa eneo hilo ikiwemo watano waliouwawa katika kambi ya wakimbizi.
Hospitali ya Al-Awada iliyoko Nuseirat imesema kwamba imepokea majeruhi kadhaa baada ya wanajeshi wa Israel kufyatua risasi kwa raia waliokuwa kwenye kituo cha misaada ya kiutu.
Jeshi la Israel halijajibu juu ya tuhuma hizo za mashambulizi katikaji ya mazungumzo ya kusaka suluhu yanayoendelea Doha, Qatar.