Mazungumzo kuhusu amani ya Gaza yafanyika Misri
6 Machi 2025Kulingana na vyanzo vya kuaminika, mazungumzo hayo yamemalizika katika hali ambayo inatoa matumaini ya kuelekea kwenye awamu ya pili ya usitishwaji mapigano huko Gaza ambayo inajumuisha kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel waliosalia mikononi mwa Hamas huku Israel ikiwaondoa kabisa wanajeshi wake katika eneo hilo.
Mazungumzo hayo kati ya wawakilishi wa Marekani, Misri na Hamas yalijadili pia kuhusu utawala ujao wa Gaza na majina ya watu wanaoweza kuuongoza Ukanda huo mara tu vita vitakapomalizika.
Misri kwa ushirikiano na mataifa ya Kiarabu iliwasilisha jana Jumatano, pendekezo kuhusu hatma ya Gaza ikisema Wapalestina wanatakiwa kusalia katika ardhi yao na kushirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa eneo hilo. Wakazi wa Gaza walionekana kufurahishwa na wazo hilo.
"Matokeo yaliyofikiwa jana ni matokeo ambayo yanawanufaisha watu wa Palestina na kujali maslahi yao. Tunatumai yataheshimiwa na kutekelezwa."
"Ni mkutano mzuri wa kilele uliozingatia maslahi ya watu wa Palestina, huku kipaumbele chake kikuu kikiwa ni ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza, kwani unahitaji kufufuliwa."
Hamas yakosoa kauli za vistisho za rais Trump
Kundi la Hamas limekosoa vitisho vilivyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump ikisema vinafanya mambo kuwa magumu katika mchakato wa mpango wa kusitisha mapigano huko Gaza. Trump alisema anatoa onyo la mwisho kwa Hamas kuwaachia mateka waliosalia la sivyo kundi hilo litasambaratishwa.
Wakati kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu hatma ya makubaliano legelege ya kusitisha mapigano huko Gaza, mkuu mpya wa jeshi la Israel, Eyal Zamir amesema mpango wa nchi yake wa kuishinda Hamas bado haujakamilika.
Soma pia: Nchi za Kiarabu zaidhinisha mpango wa kuijenga upya Gaza
Zamir anayechukua nafasi ya Herzi Halevi, aliyejiuzulu mwezi Januari kutokana na mapungufu ya jeshi kufuatia shambulio la Oktoba 7, ameyasema hayo katika hafla ya kumuidhinisha hapo jana iliyofanyika katika makao makuu ya jeshi mjini Tel Aviv na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, aliyeongeza kuwa Israel imedhamiria kupata ushindi kamili katika vita hivyo.
Kauli ya Netanyahu imetolewa siku chache baada ya viongozi wa nchi za Kiarabu kuafikiana kuhusu mpango wa dola bilioni 53 wa kuujenga upya Ukanda wa Gaza chini ya utawala wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina , mpango ambao unachukuliwa kama mbadala wa pendekezo lililokoselewa kimataifa la Rais wa Marekani Donald Trump la kuchukua udhibiti wa eneo hilo na kuwahamisha Wapalestina.
(Vyanzo: Mashirika)