Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine kuanza Istanbul
16 Mei 2025Mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine tangu mwaka 2022, yanafanyika kutokana na shinikizo la rais wa Marekani Donald Trump anayedhamiria kuvimaliza vita vibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.
Wajumbe wa pande zote tayari wamewasili nchini Uturuki. Ujumbe wa Ukraine unaongozwa na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov, utakutana na ule wa Urusi unaoongozwa na Vladimir Medinsky ambaye ni msaidizi wa rais wa Urusi. Lakini kabla ya mazungumzo hayo yatakayofanyika katika jumba la kifahari la Dolmabahce, mawaziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andriy Sybiha, wa Uturuki Hakan Fidan na wa Marekani Marco Rubio wamekutana kwa mazungumzo ya saa nzima.
Baadaye wawakilishi wa Ukraine walikutana pia kwa mazungumzo na washirika wao wa Magharibi kutoka mataifa ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Hata hivyo matumaini ya kufikia mwafaka ni madogo mno kama alivyoeleza waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio huku rais Donald Trump aliye ziarani katika nchi za Ghuba akisema hapo jana kuwa hatarajii kwamba hatua kubwa itafikiwa huko Istanbul hadi atakapokutana na rais wa Urusi Vladimir Putin.
Matumaini madogo kwenye mazungumzo hayo
Serikali ya Ukraine imesema ina mashaka na uwezo wa kuchukua hatua wa ujumbe wa Urusi uliotumwa kwenye mazungumzo hayo ikiwataka kukanusha hilo kwa kuchukua hatua ya kuafiki mpango wa usitishwaji mapigano na kuanza rasmi kwa mazungumzo ya amani.
Akiwasili mjini Tirana-Albania kushiriki mkutano wa viongozi wa Ulaya, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte amesema Putin anapaswa kuonyesha nia thabiti ya kuvimaliza vita:
"Nadhani Putin amefanya kosa kwa kuuleta ujumbe wa ngazi ya chini kwenye mazungumzo haya ukiongozwa na mwanahistoria ambaye alikuwepo kwenye mazungumzo ya mwaka 2022. Ni wazi kwamba kwa sasa jukumu liko upande wake yeye ndio anatakiwa achukue hatua. Anapaswa kuonesha nia thabiti ya kutaka amani. Kwa hivyo nadhani shinikizo lote sasa liko kwa Putin."
Maelfu ya watu wameuwawa pande zote tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari mwaka 2022 na kwa sasa Urusi inakalia karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine.
(Vyanzo: Mashirika)