Mazishi ya Edgar Lungu bado ni kitendawili
22 Julai 2025Katika hatua ya kushangaza, kundi la Progressive Forces of South Africa limejitokeza na kushinikiza kurejeshwa kwa mwili wa marehemu nchini Zambia, likidai kuwa, Lungu hafai kuzikwa Afrika Kusini kutokana na tuhuma za ufujaji wa mali ya umma zilizomkumba wakati wa uongozi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Pretoria, mratibu wa kundi hilo Bonangse Polwane, amesema ucheleweshaji wa maziko hayo ni tishio kwa heshima ya viongozi wa Afrika. Ameilaani hali hiyo akiiita uchawi wa kisiasa unaozuia mwili wa marehemu Edgar Lungu kurejeshwa Zambia.
“Tunapinga kabisa hoja kwamba mabaki ya marehemu yanaweza kutumiwa kwa uchawi wa kisiasa. Hiyo si sababu ya msingi kwa Rais wa zamani kutozikwa katika ardhi ya nchi yake mwenyewe.”
Serikali ya Zambia yafika mahakamani kuzuia mazishi ya Lungu nchini Afrika Kusini
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Mahakama Kuu ya Pretoria iliagiza serikali ya Zambia iwasilishe ombi rasmi la kurejeshwa kwa mwili huo kabla ya tarehe 3 Julai, huku familia ya Lungu ikiwekewa muda wa mwisho wa kujibu kufikia tarehe 4 Julai.
Ripoti zinaeleza kuwa familia ya hayati Edgar Lungu pia ina wasiwasi wa kurejea Zambia, ikihusishwa na mashitaka ya umiliki wa mali za kifahari zinazodhaniwa kupatikana kwa njia isiyo halali.
Familia ya Lungu inawasiwasi wa kurejea Zambia
“Hatupingani na familia ya Lungu. Tunachosema ni kwamba warudi Zambia, wasafishe majina yao, na wape nafasi watu wa Zambia kumuaga kiongozi wao.”
DW imewasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mulambo Hamakuni Haimbe kutaka kujua mchakato wa mazishi umefikia wapi, waziri huyo akadai kesi bado iko mahakamani.
Rais wa zamani wa Zambia Lungu afariki akiwa na umri wa miaka 68
Kwa sasa, bado haijafahamika wazi ni lini na wapi mwili wa Edgar Lungu utazikwa. Lakini shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa Afrika Kusini linaendelea kupamba moto huku mtoto wa Rais wa Zamani Kaweche Kaunda, akiwataka familia na serikali kufikia makubaliano ili mambo yaishe kwa amani.
“Ninaelewa maumivu ambayo familia ya Lungu inapitia. Nasi tuliwahi kupitia hali kama hiyo. Lakini ni muhimu kufikia mwafaka na serikali. Natumaini, kwa maslahi ya taifa, kuwa familia ya Lungu inapaswa ifikirie sakata hili nje ya mlengo wa wa siasa. Wananchi wa Zambia wangependa rais wao arejeshwe nyumbani.”
Hakainde Hichilema ashinda uchaguzi wa rais Zambia
Sakata la kucheleweshwa kwa maziko ya Rais wa zamani Edgar Lungu sasa limegeuka kuwa kama maombolezo yasiyoisha, na pia limechukua sura ya kisiasa, kufuatia kauli ya mwanasiasa kutoka chama cha marehemu, cha Patriotic Front, akiwataka Wazambia kutomrudisha madarakani Rais Hakainde Hichilema katika uchaguzi ujao, kwa madai kwamba ameshindwa kuwaheshimu watangulizi wake.