Mazingira vs. uchumi: Je, Ujerumani inapaswa kuchagua?
12 Februari 2025Ajira, mapato na uchumi wa Ujerumani unaodorora ni mada kuu kwa vyama vya siasa vya nchi hiyo kuelekea uchaguzi wa mwezi huu, huku vingi vikilenga hatua za kulinda mazingira.
Friedrich Merz — mwenyekiti wa Chama cha Christian Democratoc Union (CDU) cha mrengo wa wastani wa kulia na anayetarajiwa kuwa kansela ajaye — amesema ataondoa mitambo ya makaa ya mawe na gesi tu ikiwa haitadhuru sekta ya viwanda ya Ujerumani.
Hata vyama vinavyounga mkono hatua za kulinda mazingira havizungumzi sana kuhusu mada hiyo kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa 2021.
Soma pia: Scholz na Merz wanyukana kwenye mdahalo wa Televisheni kuelekea uchaguzi Ujerumani
Hali hii imewafanya baadhi ya wataalamu kuwa na wasiwasi kwamba uchumi unapewa kipaumbele kuliko mazingira, ingawa utafiti wa Climate Alliance, muungano wa asasi za kiraia nchini Ujerumani, umebaini kuwa wananchi wengi wangependa hatua zaidi zichukuliwe kulinda mazingira.
"Tayari inaonekana kwamba kuelekea uchaguzi wa shirikisho, uchumi na mazingira vinawekwa kwenye mizani dhidi ya kila mmoja," alisema Claudia Kemfert, mchumi na mtaalamu wa nishati kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Ujerumani (DIW).
Je, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ndizo zinazoathiri uchumi wa Ujerumani?
Kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, uchumi wa Ujerumani, ambao ni mkubwa zaidi barani Ulaya, umepungua kwa miaka miwili mfululizo.
Uchumi wake unaotegemea viwanda na mauzo ya nje umekumbwa na changamoto za bei kubwa za nishati, mahitaji duni ya ndani, na biashara dhaifu duniani. Wakati huohuo, sekta yake ya magari — ambayo ni mhimili wa uchumi wake — imetangaza kupunguza wafanyakazi kwa wingi, huku mauzo na faida vikizidi kushuka.
Hata hivyo, sera za kupambana na mabadiliko ya tabianchi si sababu ya mdororo huu wa kiuchumi, anasema Gunnar Luderer, mwanasayansi anayejikita katika mabadiliko ya nishati katika Taasisi ya Utafiti wa Athari za Tabianchi ya Potsdam. "Tatizo la uchumi wa Ujerumani ni la kimuundo, na lina mizizi mirefu zaidi."
Soma pia: Jinsi Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alivyopoteza umaarufu wake
Amesema mojawapo ya matatizo makuu ni utegemezi wa Ujerumani kwa gesi kutoka Urusi, ambayo ilikuwa ghali kuachana nayo baada ya uvamizi wa Ukraine. Bei kubwa za nishati zimeathiri uchumi kwa kuongeza gharama za uzalishaji kwa viwanda vinavyotumia nishati nyingi, kama vile sekta ya chuma na kemikali, pamoja na kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.
Mfumo wa uchumi wa Ujerumani pia umeonyesha udhaifu wake kutokana na ushindani wa kimataifa na shinikizo kutokana na upanuzi wa China kwenye masoko mapya kama sekta ya magari ya umeme (e-mobility), kulingana na Gunnar Luderer.
"Watengenezaji wa magari wa Ujerumani walikuwa wanakwenda pole mno na wamechelewa sana kuingia kwenye mwelekeo huu mpya," alisema, akiongeza kuwa sasa nchi inalipa gharama ya kuchelewa huko.
Wakati mauzo ya magari ya umeme yameshuka Ulaya na Marekani, nchini China yamepanda kwa kasi, yakifikia karibu asilimia 50 ya magari yote yanayouzwa.
Ajira na rursa zinazopuuzwa
"Madai kwamba hatua za kulinda mazingira zinaathiri uchumi wa Ujerumani si sahihi," alisema Claudia Kemfert, ambaye anasisitiza kuwa sera bora za kulinda mazingira huleta faida kubwa za kiuchumi ambazo mara nyingi hudharauliwa.
Alisema uwekezaji katika nishati jadidifu, magari ya umeme, ukarabati wa majengo kwa kuzingatia ufanisi wa nishati, na ufanisi wa nishati katika sekta ya viwanda ni hatua zinazohitaji uwekezaji mkubwa, ambao huunda thamani na ajira.
Soma pia: Ujerumani imevuka kiwango chake cha ikolojia kwa mwaka
Sekta ya nishati jadidifu tayari imetengeneza ajira karibu 400,000 nchini Ujerumani, huku ajira zikiongezeka kwa karibu asilimia 15 kati ya 2021 na 2022, hasa katika sekta za nishati ya jua na pampu za joto.
"Ikiwa Ujerumani itaweka uchumi dhidi ya mazingira, kuna hatari ya kupoteza ajira, kushuka kwa ushindani, na gharama kubwa za mafuta ya kisukuku," alionya Kemfert.
Kwa kuzingatia nguvu ya uchumi wa Ujerumani katika utengenezaji wa mashine na magari, kuna fursa nyingi za kiuchumi kwa nchi kuwa kinara wa teknolojia ya kijani kama vile nishati ya upepo, pampu za joto, magari ya umeme, na mifumo mahiri ya kudhibiti matumizi ya nishati, alisema Luderer.
Shirikisho la Viwanda la Ujerumani (BDI), ambalo linawakilisha kampuni za kemikali, uhandisi, na umeme, nalo limeonyesha kuunga mkono sera za mazingira, likisisitiza kuwa teknolojia za kijani zitakuwa msingi wa mafanikio ya viwanda vya Ujerumani katika siku zijazo.
Wataalamu pia wanasema kuwa uwepo wa nishati jadidifu katika mchanganyiko wa nishati umezuia kupanda kwa kasi kwa bei ya umeme licha ya kupanda kwa bei ya gesi.
Niklas Höhne, mwanasayansi na mwanzilishi wa taasisi ya utafiti ya NewClimate, anasema kuwa bei ya umeme inasukumwa juu na vyanzo vya nishati vya gharama kubwa zaidi kwenye mfumo wa nishati, ambavyo mara nyingi ni mitambo ya gesi, huku gharama za nishati jadidifu zikiendelea kushuka duniani kote.
"Hivyo basi, ni utegemezi wetu kwa mafuta ya kisukuku unaosababisha kupanda kwa bei ya umeme, na si upanuzi wa nishati jadidifu," alisema Höhne.
Gharama za kutochukua hatua na kutokuwa na uhakika wa kisera
Vyama kadhaa vya kisiasa vimesema vitafuta sheria mpya ya ujenzi inayolenga kuondoa mifumo ya kupasha joto inayotumia mafuta ya kisukuku, ambayo ilianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka wa 2023. Pia vimepanga kupinga marufuku ya magari mapya yanayotumia injini za mwako ndani ya Umoja wa Ulaya kufikia mwaka 2035.
Kutokuwa na uhakika kwa sera za kisiasa kunakwamisha mipango ya muda mrefu kwa biashara, alisema Stefanie Langkamp, mkurugenzi mtendaji wa masuala ya siasa katika Climate Alliance.
"Kila unapozungumza na viwanda au vyama vya wafanyakazi, wanasema kuwa hili ni jambo muhimu sana kwao kupanga mustakabali wao," alisema.
Soma pia: Kizazi cha mwisho waitisha maandamano ya tabianchi Ujerumani
Langkamp alitoa mfano wa sekta ya pampu za joto, ambayo tayari imeajiri na kutoa mafunzo kwa mafundi wapya, pamoja na kununua vifaa ili kupanua uwezo wake.
"Iwapo hatutawekeza katika hatua za kulinda mazingira leo, basi tutakumbwa na madhara makubwa sana, siyo tu kwa uchumi, bali pia kwa gharama zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi," alionya Langkamp.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la sayansi Nature umegundua kuwa hasara za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi duniani ni mara sita zaidi ya fedha zinazohitajika kuwekeza katika hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kuweka joto la dunia chini ya nyuzi 2°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Nchini Ujerumani, matukio mabaya ya hali ya hewa kama dhoruba na mafuriko yanakadiriwa kusababisha hasara ya euro bilioni 7 katika mwaka wa 2024 pekee.
Dunia inaelekea katika uchumi usiotegemea kaboni katika miongo ijayo, na maendeleo makubwa tayari yamefanyika katika sekta za nishati jadidifu, pampu za joto, na magari ya umeme, alisema Langkamp.
"Huenda kasi ikawa tofauti kati ya nchi au sekta mbalimbali, lakini bado huu ni mwelekeo wa dunia nzima, na hautasimama," aliongeza.
"Hivyo basi, ikiwa hatutawekeza katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sasa, basi tutakumbwa na matatizo makubwa ya ushindani baadaye."
"Laiti tungechagua njia pekee kwa uchumi wa Ujerumani, basi ni kuikumbatia kwa dhati changamoto na fursa za mpito wa kijani," alisema Luderer. "Hakuna njia ya kurudi nyuma. Hatari kubwa zaidi kwa uchumi wa Ujerumani ni kuchelewesha mpito huu au kutegemea mifumo ya zamani ya biashara isiyofanya kazi tena."