Mawaziri wa uhamiaji wa Ulaya wazungumzia uhamiaji
23 Julai 2025Mkutano huo uliowakutanisha mawaziri wa Umoja wa Ulaya umeangazia changamoto na mwelekeo mpya wa sera za uhamiaji barani Ulaya hasa katika kipindi cha ongezeko la wakimbizi kutoka maeneo yenye mizozo.
Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakikutana mjini Copenhagen, mji mkuu wa Denmark, nchi inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya, kujadili njia za kuongeza safari za kurejesha makwao raia wa mataifa ya kigeni.
Mazungumzo hayo ni muendelezo wa mkutano wa awali uliofanyika nchini Ujrumani, ambapo baadaye mipango kadhaa ya kuzuia au kuwarejesha makwao waombaji hifadhi waliokataliwa maombi yao na wahamiaji wengine wanaoonekana kuwa hawatakikani, iliridhiwa.
Saual la kuwarudisha kwao raia wa kigeni limeshinikiwa na Denmark hususan katika miaka ya hivi karibuni. Uongozi wa nchi hiyo uliandaa barua ya wazi iliyovitaka vyombo vya kisheria na utetezi wa haki za binadamu Ulaya vizingatie upya kuruhusu safari zaidi za ndege za kuwarejesha raia wa kigeni katika nchi zao.
Denmark pia imeweka wazi bayana kwamba inanuia kutumia kipindi hiki inachokalia kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya, kuushinikiza umoja huo kufungua njia zaidi za kuwaondosha watu, na ujenge vituo vya ziada nje ya himaya yao vya kuwapokea raia wa kigeni watakaofukuzwa Ulaya.
Denmark si nchi pekee inayopigania mageuzi
Denmark sio nchi pekee ya Ulaya inayotaka mageuzi katika mfumo wa uhamiaji na uombaji hifadhi. Viongozi katika nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya wameitaka halmashuri kuu ya Ulaya, ifungue njia zaidi za kuwarejesha wageni makwao, na imewakubalia kwa kuanzisha mchakato wa kisheria kwa nchi moja moja mwanachama kufuatilia mipangilio ya ujenzi wa vituo vya kuwapokea wale wanaofukuzwa.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt amewasilisha wazo jana Jumanne kwamba kundi dogo la nchi za Umoja wa Ulaya huenda zikaungana kuanzisha vituo vya kuwapokea waomba hifadhi watakaokataliwa katika nchi zilizo nje ya Umoja wa Ulaya. Lengo ni kuwarejesha wahamiaji waliokataliwa maombi yao katika nchi wanakotokea kwa haraka zaidi.
Akiwasili katika mkutano wa Copenhagen Dobrindt alisema kuna fursa nyingi nje ya Ulaya kuanzisha vituo vya aina hiyo na nchi washirika. "Tunataka kulifanya kuwa rasmi lengo hili," Donbrindt aliwaambia waandishi habari.
Mtazamo mpana wa pamoja wa Umoja wa Ulaya na mpango wa nchi moja moja wanachama wa umoja huo yote yanawezekana, alisema waziri huyo wa Ujerumani. "Sitaki nifutilie mbali uwezekano wa Ujerumani kujiunga na nchi nyingine," alisema.
Uhamiaji usio na mpangilio
Pamoja na suala la kuwarejesha wahamia waliokataliwa maombi yao katika nchi zao wanakotokea, mazungumzo ya Copenhagen yanatuwama juu ya hatua dhidi ya uhamiaji usio na mpangilio na mapambano dhidi ya uhalifu wa kupanga na ulanguzi wa dawa za kulevya. Nchi wanachama pia zinapania kuwa na jukumu kubwa na imara zaidi kwa wakala wa ulinzi wa mipaka Frontex.
Dobrindt aliwahi kupigania mtazamo mkali zaidi kuhusu sera ya uhamiaji katika mkutano uliofanyika Bavaria Ijumaa wiki iliyopita na mawaziri wa mambo ya ndani kutoka Austria, Ufaransa, Denmark, Poland na Jamhuri ya Cheki, likiwemo pia suala la safari zaidi za kuwarejesha wahamiaji makwao, hata kuelekea nchini Syria na Afghanistan.
Mbali na masuala ya uhamiaji, mawaziri pia wanapanga kujadili kuhusu jinsi Umoja wa Ulaya unavyoweza kufanywa kuwa imara zaidi kukabiliana na migogoro mbalimbali kama vile majanga asili au masuala kama vile kukatika kwa teknolojia ya habari na mtandao wa mawasiliano wa intaneti.
Mabadiliko ya sera yanaandaliwa
Wakati huo huo, mabadiliko ya kisera yanaandaliwa yatakayoondosha mfumo unaozuia watu wasirudishwe mahali ambako hawana mafungamano nako, kwa maana kwamba kule wanakotokea ama kule waliko na ukazi.
Kuondoa mfumo huo kutafungua mlango kuwezesha watu warudishwe makwao kirahisi zaidi, kwa kuwa nchi nyingi ambako watu wanatokea ima haiziwakubali watu waliorudishwa kwa nguvu ama kwa sababi nyingine za kimipango hazitaki ama haziko tayari kufanya hivyo.
Halmashauri ya Ulaya katika siku za hivi karibuni imefanya mageuzi muhimu katika jinsi inavyopang akutumia fedha za maendeleoe nje ya Umoja wa Ulaya kuzichochea nchi zaidi zikubali kuwakubali raia wao wanaorudishwa makwao.
Katika pendekezo la bajeti mpya ya halmashauri hiyo kuna kipengele kinachopendekeza kwamba fedha kwa ajili y amaendeleo zinaweza kuchukuliwa kutoka kwa nchi ambazo zitakaa kutoa ushirikiano - ingawa hii haitazihusu fedha zilizotengwa kwa ajili ya msaada wa kibinadamu.
Pendekezo hilo pia limetambua umuhimu wa kuingeza ufadhili kwa ajili ya ulinzi wa mipaka na miundombinu, huku likiwacha fedha chache kwa ajili ya mipango ya uhamiaji na kuwajumuisha wageni katika jamii.
Hatua hizi zote - pamoja na mipango kama hii inayoonekana Uingereza, inapendekeza kuwa katika siku za usoni sera y auhamiaji ya Ulaya itajikita zaidi katika kuimarisha usalama wa mipaka na kuongeza safari za kuwarejesha raia wa kigeni katika nchi zao, kinyume na awali ambapo sera iliyotawala Ulaya ilikuwa kuwaruhusu watu waingine na kuchakata maombi yao ya kutaka uhamiaji.