Mawaziri wa NATO wajadili sharti la uwekezaji wa ulinzi
15 Mei 2025Akizungumza mjini Antalya, Uturuki, Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte amesema uwekezaji zaidi na vifaa vya kijeshi vinahitajika kukabiliana na kitisho kinachotolewa na Urusi na ugaidi, lakini pia na China ambayo imekuwa suala la wasiwasi kwa Marekani.
Soma pia: NATO yaahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine
Rutte amewaambia waandishi kuwa mara vita vitakapomalizika nchini Ukraine, Urusi inaweza kuunda upya vikosi vyake ndani ya miaka mitatu hadi mitano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anasisitiza kuwa sharti la uwekezaji la Marekani linahusu kutumia fedha kwenye mambo yanayohitajika kukabiliana na vitisho vya karne ya 21.
Mjadala kuhusu gharama ya ulinzi unapamba moto kabla ya mkutano wa kilele wa Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wenzake wa NATO nchini Uholanzi Juni 24-25. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul amesema Berlin iko tayari kulitekeleza sharti hilo la Trump akisema ni suala muhimu.