Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waiunga mkono Ukraine
12 Agosti 2025Kauli mbiu ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ilitolewa na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo Kaja Kallas aliyesema kuwa mshikamano wa kuisaidia Ukraine na kuzidisha shinikizo kwa Urusi vinahitajika ili kumaliza vita na kuzuia uchokozi wowote wa baadaye wa Urusi barani Ulaya.
Kallas amesema Umoja huo unaandaa kifurushi kipya na cha 19 cha vikwazo kwa Urusi, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi. Kallas amesisitiza kwamba kwa kuwa Urusi haikukubali mpango wa kusitisha mapigano bila masharti, hakuna makubaliano yoyote yanayopaswa kujadiliwa bila kuishirikisha Ulaya:
"...Ni muhimu kuhakikisha hakuna kitu kinachoamuliwa bila ya Ukraine na Ulaya kushirikishwa. Kwa sababu yote haya yanahusu usalama wa Ukraine na Ulaya, kwa hivyo hakuna kitu kinachoweza kuafikiwa nyuma ya migongo yetu. Hilo ndio jambo muhimu zaidi. Jambo la pili ambalo ni muhimu, ni kwamba usitishaji wa mapigano bila masharti unapaswa kutangulia mazungumzo yoyote. Ikiwa mabomu bado yanafyetuliwa, ni vigumu kuendelea kutathmini namna ya kusonga mbele. Hayo huenda ndio mambo muhimu...'”
Kauli ya Trump na mipango ya viongozi wa Ulaya
Hata hivyo Trump amesisitiza usiku wa kuamkia Jumanne kuwa mkutano wake na Putin siku ya Ijumaa huko Alaska hauna nia ya kufikia makubaliano yoyote, bali ni wa kujadili namna ya kuvimaliza vita vya Ukraine vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hata hivyo Trump amesema angependelea kushuhudia usitishwaji mapigano na mpango utakaokubalika na pande zote lakini akasisitiza kuwa Moscow na Kiev zitatakiwa kuachia baadhi ya sehemu za ardhi.
Kwa kuhofia kwamba huenda Putin akaungana na Trump kulazimisha mapango wa amani usiokubalika, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameitisha mkutano ambapo viongozi wa Ulaya kutoka mataifa ya Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Poland na Finland wanapanga kuzungumza siku ya Jumatano kwa nyakati tofauti na marais Zelensky wa Ukraine na Trump wa Marekani.
//DPA, AFP, AP