Bolsonaro hakukiuka marufuku ya mitandao ya kijamii
23 Julai 2025Mawakili wa rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro wameiambia mahakama ya juu kabisa ya nchi hiyo kwamba kiongozi huyo hakukiuka agizo la mahakama katika mtandao wa kijamii, baada ya jaji wa koti hiyo kumtuhumu kwa kuiendea kinyume amri hiyo ya mahakama na kutaka maelezo kutoka kwa mawakili.
Katika waraka uliotumwa kwa jaji wa mahakama hiyo Alexandre de Moraes, anayesimamia uchunguzi wa madai kwamba Bolsonaro alipanga njama ya mapinduzi, mawakili wa Bolsonaro wameiomba mahakama ifafanue upana wa marufuku inayohusu mitandao ya kijamii.
Moraes aliamuru marufuku dhidi ya mtandao wa kijamii Ijumaa iliyopita, pamoja na kuamuru avae bangili ya kifundo cha mguu ili aweze kufuatiliwa, miongoni mwa hatua nyingine.
Siku ya Jumatatu Morae alimtuhumu Bolsonaro kwa kupuuza agizo la mahakama kwa kuhojiwa na waandishi habari na video zake baadaye zikachapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya vyombo vyao vya habari.
Jaji huyo amewataka mawakili watoe maelezo la sivyo atatoa waranti wa kumkamata Bolsonaro.