Mauaji ya wanawake yaongezeka nchini Kenya
10 Aprili 2025Ripoti hiyo inayoonyesha taswira ya kuhuzunisha inabainisha kuwa idadi kubwa zaidi ya mauaji ya wanawake ilisajiliwa mwezi wa Machi ambao ulikuwa na visa 44, ukifuatiwa na Januari iliyorekodi vifo 43 na Februari vifo 42. Asilimia 60 ya visa hivyo vinaonesha kuwa waathiriwa waliuawa na jamaa zao wa karibu. Nairobi iliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mauaji ya wanawake kwa visa 19, ikifuatiwa na majimbo ya Kiambu iliyoandikisha vifo 17, Kilifi 16, na Trans Nzoia 13.
Katika kaunti za West Pokot na Nandi, waathiriwa wote wa mauaji walikuwa wanawake, huku Busia ikiripoti wanawake saba kati ya waathiriwa wanane. Takwimu hizi zilitolewa wakati wa mkutano wa Jopo Kazi la Kiufundi kuhusu Ukatili wa Kijinsia na Mauaji ya Wanawake ambao pia uliashiria mwisho wa mashauriano na wadau wanaoshughulikia ukatili wa kingono na kijinsia na mauaji ya wanawake kote nchini.
Utafiti: Karibu wanawake 200 waliuawa Kenya mwaka 2024
Nancy Baraza ni mwenyekiti wa jopo kazi hilo na amesema kinachotakiwa kufanywa ni familia kuishi kwa mshikamano, wazazi kuishi na watoto vizuri na vyombo vya usalama viendelee kuwa macho.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mwaka jana, wanawake 579 waliuawa, ongezeko kutoka visa 534 mwaka 2023 na 526 mwaka 2022. Wanaume walihusika katika asilimia 85 ya mauaji hayo, wanawake asilimia 10, huku asilimia 5 iliyosalia ya watuhumiwa haijajulikana.
Je nini kinaweza kufanyika kukomeza madhila hayo kwa wanawake?
Ili kuboresha uratibu na mwitikio, Kituo cha Utafiti na uhalifu kilipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa data wa pamoja unaopatikana kwa wadau wote husika na kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji ili kukomesha tamaduni kandamizi zinazochochea ukatili dhidi ya wanawake.
Hii ni pamoja na matumizi ya tuhuma za uchawi kuhalalisha mauaji, hasa yanayowalenga wanawake wazee kuhusu ardhi. Mkuu wa Masuala ya Kisheria katika Huduma ya Polisi nchini Amos Omuga, alipendekeza kuanzishwa kwa mahakama za haki ya kijinsia katika kila kaunti ili kuharakisha usikilizaji wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake.
''Kile kinachohitajika kufanyika ni kuboreshwa kwa mifumo iliyopo, ili masuala hayo yaangaziwe. Pengine tunahitaji kuweka muda wa kuyashughulikia na kuyapa ufumbuzi,'' alisema Omuga.
Wanaharakati nchini Kenya waihimiza serikali ikomeshe mauaji ya wanawake
Pia aliunga mkono matumizi ya mfumo wa kidijitali kutumika kama zana za kuripoti visa vya unyanyasaji ili kuruhusu waathiriwa kuwafahamisha maafisa wa usalama kwa haraka na kwa siri. Ripoti hiyo imepokelewa kwa maoni mseto, huku Wakenya wakiwalaumu polisi kwa visa hivyo. Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa wahalifu wengi walikuwa wanawajua waathiriwa. Silaha kali kama visu na mapanga zilitumika katika asilimia 40 ya mauaji, vitu butu asilimia 30, kunyongwa asilimia 15, na silaha za moto asilimia 5 ya visa.